Harmonize aiangukia Basata kurudisha tuzo za muziki

Muktasari:

"Bila tuzo ni sawa na kujitekenya na kucheka mwenyewe na kutumia nguvu kuwaaminisha watu kuwa wewe ni zaidi" ameeleza Harmonize

Mkali wa wimbo wa ' Fall in love' unaotamba kwa sasa, Harmonize ametuma ujumbe kwa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kuhusu umuhimu wa kurudi kwa tuzo za muziki nchini Tanzania.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram katika kipengele cha Insta story leo Jumamosi Julai 4, 2020, msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Rajab Abdul, ameandika hivi;

"Kutokuwepo tuzo kunapunguza thamani ya muziki Tanzania, maana sasa hivi tumebakia kushindana YouTube tu. Ngoma yako isipofikisha watazamaji milioni moja kwa siku mbili basi hiyo ngoma si bora hali inayotupelekea wasanii kutumia nguvu kubwa katika promotion, kulipia wadhamini ili tupate watazamaji wengi. Hiyo inatumaliza ubongo na inaenda kuathiri vizazi na vizazi”

"Basata, tuzo zina heshimisha zaidi uwepo wa baraza maana sasa hivi baadhi wakisikia jina Basata tunaogopa kabisa kwa sababu hakuna kitu kinaliweka baraza na wasanii karibu kupitia tuzo” ameeleza Harmonize

Tumaini letu ni Basata pekee kupitia Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, Baba yetu Harrison Mwakyembe tunaomba kuwasilisha.

Harmonize aliyeibuliwa na kibao cha Aiyola, ameendelea kuandika "Bila tuzo ni sawa na kujitekenya na kucheka mwenyewe na kutumia nguvu kuwaaminisha watu kuwa wewe ni zaidi.

Ni ngumu kujua kazi zako zina mapokezi gani kwa sababu unaowaona wakijirekodi video na kukutumia ni mashabiki zako tu wale wasio mashabiki zako mtazamo wao huujuwi.

“Tuzo ni kipimo cha msanii yeyote duniani kujua wapi umelegeza ili next ukaze ukikosa zinakufanya ujitambue na ujue levo yako lakini pia zinatia moyo na hamasa ya kufanya kazi” alihitimisha Harmonize

Hata hivyo, Moja ya tuzo ambazo ziliwahi kupata umaarufu nchini ni tuzo za Kili ambapo Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema tuzo hizo wana mpango wa kuirudisha endapo atapatikana mdhamini kwani ina faida kwa wasanii wa muziki ikiwemo kujuliakana na kupata fursa za kufanya kazi na wasanii wengine wa ndani na nje ya nchi.