Harambee Stars yanusa AFCON kimtindo

Muktasari:

Ushindi walioupata Kenya dhidi ya Ethiopia, ugani Moi Kasarani, unaifanya Kenya kujisogeza karibu na mlango wa kuingilia 2019 AFCON, kwani hivi sasa wanaongoza Kundi F, wakiwa na pointi saba.

Nairobi, Kenya. Hatimaye Wakenya wanaweza kuanza kuota ndoto za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14, baada ya kujikita kileleni mwa Kundi F, kufuatia kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia ugani MISC Kasarani.

Ukiwa ni mchezo wa marudiano, baada ya kulazimisha sare ya 0-0 huko Addis Ababa, vijana wa Sebastien Migne wakiongozwa naNahodha Victor Wanyama walijitosa uwanjani wakifahamu fika kuwa wanahitaji ushindi na sio vinginevyo, huku Ethiopia nao wakipambana kupata matokeo.

Licha ya Ethiopia kuonesha uhai tangu kipindi cha kwanza huku juhudi za Eric Johanna na Eric Ouma ‘Marcelo’ (dakika ya 4), kutozaa matunda, Kenya ikijivunia sapoti kubwa ya mashabiki zaidi ya 50,000, ilijipatia bao la kuongoza, likiwekwa kimiani na Michael Olunga, katika dakika ya 23, ikiwa ni dakika chache baada ya Getane Kadebe wa Ethiopia kukosa nafasi ya wazi.

Olunga alitumia uzoefu kukwapua mpira ambao ulikuwa umeelekezwa kwa nyota wa IF Bromma, Eric Johanna na kuachia shuti kali lilitiga moja moja wavuni na kumuacha kipa wa Ethiopia, Samson Asefa akichupa bila mafanikio.

Dakika tano baadae, Johanna akazamisha bao la pili, akipokea pasi nyepesi kutoka kwa kiungo wa Gor Mahia, Francis Kahata, aliyepokea krosi kutoka Marcelo ambaye alikuwa moto wa kuotea mbali katika mchezo huo wa Kundi F.

Zikiwa zimesalia dakika chache kipindi cha kwanza kimalizike, Stars walijikuta wakishindwa kutumia nafasi ya kuongeza bao baada ya mpira wa kona uliochongwa na Johanna kumpapasa kipa wa Ethiopia huku Brian Mandela akishindwa kuchangamka haraka kuweka mpira kambani. Kipindi cha kwanza kikamalizika, Stars wakiwa mbele 2-0

Katika kipindi cha Pili, vijana wa Sebastien Migne walitawala mchezo kwa zaidi ya asilimia 56, huku safu ya kiungo lililokuwa likiongozwa na Wanyama akishirikiana na Kahata.

Kufuatia mchezo mzuri, Kenya ilijipata ikiwachanganya Wahabeshi, ambapo Johanna aliangushwa ndani ya boksi. Kenya ikazawadiwa penalti, iliyochongwa na Wanyama na kuipatia Stars bao la tatu na la ushindi.

Kikosi cha Harambee Stars

Patrick Matasi (kipa), Abud Omar, Philemon Otieno, Brian Mandela, Musa Mohamed, Dennis Odhiambo, Victor Wanyama (nahodha), Eric Johanna,  Francis Kahata, Eric Ouma, Michael Olunga

Akiba: Faruk Shikalo, Brian Bwire, Bernard Ochieng, Joash Onyango, David Ochieng, Anthony Akumu, Johanna Omollo, Ismael Gonzalez, Paul Were, Ovella Ochieng, Piston Mutamba, Allan Wanga .

Kikosi cha Ethiopia

Samson Asefa (kipa), Getaneh Kebede , Aschalew Tamene, Anteneh Tesfaye, Mulualem Mesfen, Ahmed Reshad, Gatoch Panom, Shemeles Bekele, Abdulkerim Mohamed, Dawa Hotessa, Shemket Gugesa.

Akiba:  Shanko Balcha, Mujib Kasim, Henok Gebra, Kastro Amaye, Amesalu Telahune, Omod Okwury, Abel Yalew, Beneyam Demte, Adis Giday, Amanuel Yohannes, Kenyan Markene, Tyson Merya.