Harambee Stars, kuweka kambi Ufaransa wakifuzu Afcon

Muktasari:

Kama ikifanikiwa kutinga fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, yatakayofanyika mwakani, nchini Cameroon, itakuwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo baada ya miaka 14. Mara ya mwisho ilikuwa ni fainali za mwaka 2004, chini ya ukufunzi wa Jacob ‘Ghost’ Mulee.

Nairobi, Kenya. Oktoba 14, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, ilifanikiwa kuongeza matumaini ya kujikatia tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la mataifa ya Afrika, 2019 AFCON, kwa kuitandika Ethiopia mabao 3-0.

Ushindi huo ulimaanisha kuwa sasa Kenya, inaongoza kundi F, baada ya kufikisha pointi saba, pointi tatu juu ya Ethiopia inayoshika nafasi ya pili na Ghana inayoshika nafasi ya tatu na pointi zake tatu.

Mechi inayofuata, itakuwa dhidi ya Black Stars, ambapo kama vijana wa Sebastien Migne watafanikiwa kushinda au kulazimisha sare ya aina, watakuwa katika nafasi nzuri ya kuanza kuota ndoto za kwenda Cameroon kama sio kujiweka karibu na uwanja wa ndege kabisa.

Sasa basi, Habari njema kutoka katika ofisi za Shirikisho la Soka nchini (FKF), ni kwamba, endapo Harambee Stars itafanikiwa kukwepa kizingiti cha Ghana huku pia ikiiombe Sierra Leone mabaya, na kufuzu AFCON, Kambi ya maandalizi yataandaliwa nchini Ufaransa.

Unashangaa? Kwa mujibu wa Rais wa FKF, Nick Mwendwa, Shirikisho hilo limejipanga kuhakikisha kuwa, Stars inahamishia kambi yake nchini Ufaransa kwa kipindi cha wiki, kujiandaa na michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika.

 “Tumejipanga kuhakikisha timu inakuwa sawa kabla ya kwenda Cameroon, hiyo ni kama tutafanikiwa kufuzu. Tunachotakiwa kufanya ni kupata pointi dhidi ya Ghana na Sierra Leone. Tukifanikiwa katika hilo, nawahakikishia kuwa tutaweka Kambi nchini Ufaransa,” alisema Mwendwa.

Hata hivyo, Kenya inaweza ikajikatia tiketi ya kuelekea Cameroon mapema zaidi, kama Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ile ya Afrika (CAF), zitaendelea kushikilia msimamo wa kuifungia Sierra Leone. Kenya itakuwa inahitaji sare dhidi ya Ghana, huku ikiiombea Ghana iifunge Ethiopia, kusonga mbele.