Harambee Stars: Waleteni tu hao Algeria

Muktasari:

  • Kenya ipo Kundi C pamoja na Tanzania, Algeria, Senegal katika fainali hizo za Afrika zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19

Nairobi. KIKOSI cha Harambee Stars kiliwasili salama mjini Misri, Cairo tayari kuanza kibarua cha AFCON 2019 na mechi yao itakuwa Jumapili hii dhidi ya Algeria.

Wachezaji kadhaa wanaotarajiwa kuunda ‘First 11’ ya Kocha Mfaransa Sebastian Migne wamemimina mitazamo yao kuhusu mustakabali wa timu hasa baada ya kambi ya mazoezi ya wiki mbili kule Paris Ufaransa.

Wanyama: tupo kushindana sio kushiriki

Kiungo huyo mkabaji na nahodha kasema pamoja na Kenya ni mojawepo ya timu inayotajwa limbukeni kwenye kundi lao C, wapo kule kutoa ushindani na sio kushiriki.

“Kila mechi kwetu ni fainali, hatuendi kushiriki tu. Tupo vizuri hasa ukizingatia zile mechi mbili za kirafiki tulizocheza sioni kwa nini hatutasumbua” akasema.

Kahata: kundi gumu, hatufai kuhata

Naye kiungo mbunifu katia sauti lake kuhusu mustakabali wa timu akikiri wapo kwenye kundi gumu na ili kutoboa, itabidi wawe wajanja.

Kahata anasisitiza hesabu zao ni kuhakikisha hawapotezi dhidi ya miamba wa kundini na kamwe hawafai kuhata au itakuwa imekula kwao.

“Ni kundi gumu ukiliangalia na mpango tulionao ni kujitahidi kupata angalau alama moja kutoka kwa Senegal na Algeria. Tukifanikisha hilo basi tutakuwa kwenye nafasi nzuri sana kutinga  16 bora.”

Matasi: Tukiwakazia, tuko fiti

Kwa mtazamo wake kipa nambari moja, Patrick Matasi, ujanja kwenye kundi C ni kuhakikisha wapinzani hawafungi.

Kocha Migne amekuwa akisifia kuimarika kwa safu yake ya ulinzi  na ndiko  iliko imani ya Matasi.

“Cha muhimu kwenye hatua ya makundi ni kuwakazia wasitufunge bao sababu huwezi jua mambo yatakwenda vipi mwishoni ukizingatia sasa kuna uwezekano wa timu tatu kufuzu kutoka katika kundi. Kuna ile nafasi ya ‘best looser’ na ndio sababu hatufai kufungwa.”

Wikendi kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya DR Congo Matasi alikashifiwa kwa blanda yake iliyosababisha wapinzani kupata bao la kusawazisha.

Ni kosa lililoonekana kujirudia baada ya kulifanya tena dhidi ya Ghana walipolimwa 1-0. Hata hivyo Matasi kaahidi kurekebika na kuwa makini katika dimba hili, ajitetea kwa kusema kutokea kwa kosa huwa sio jambo la makusudi.

Olunga: Tushaiva mbona

Kwa straika tegemeo Miachel Olunga anaamini  kambi ya mazoezi ilizaa matunda na kikosi kishaiva na kipo  tayari kufanya mambo.

“Maandalizi yamekuwa mazuri. Yale matokeo dhidi ya Congo yalikuwa yakuridhisha, hii ina maaa tushaiva na tuko tayari kushindana. Langu mimi litakuwa kusaka nafasi za kufunga tu.”