Hapa hawatoshi mboga

Thursday September 13 2018

 

WAKATI mastaa Gareth Bale na Luis Suarez walipoonyesha soka la viwango vya juu kwenye vikosi vya Tottenham na Liverpool, kilichoonekana kilikuwa ni suala la muda tu kabla ya wakali hao kunasa dili za maana na zenye pesa nyingi kujiunga katika klabu kubwa.

Hilo ndilo lililotokea, Bale alikwenda kujiunga na Real Madrid kwa Pauni 85 milioni na Suarez alitua Barcelona kwa Pauni 75 milioni. Si kwamba ni kuzikosea heshima klabu hizi, ila ni ukweli wachezaji hawa watano viwango vyao vipo juu sana kuliko timu hizo wanazochezea kwa sasa.

5.Mohamed Salah (Liverpool)

Mohamed Salah alikuwa matata kwenye kikosi cha Liverpool msimu uliopita. Alicheza soka la kiwango cha juu sana lililomfanya azungumzwe sasa anakwenda kupora utawala wa kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Lakini kinachosikitisha Salah yupo kwenye timu ambayo haishindanii ubingwa. Yupo kwenye timu ambayo ikimaliza kwenye nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England yenyewe inahesabu kuwa ni mafanikio makubwa kuliko kubeba mataji kitu ambacho ndicho kinachozingatiwa kwenye timu kubwa kama za Barcelona na Real Madrid.

4.Wilfred Zaha (Crystal Palace)

Zaha alikumbwa na maumivu ya goti mara mbili tofauti msimu uliopita, lakini bado ameweza kufunga mabao matano na kuasisti manne katika mechi 24 za ligi alizoichezea Crystal Palace.

Ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa hakika na anapokosekana kwenye kikosi chake pengo lake linaonekana. Kwa uwezo wa Zaha si mchezaji wa kuendelea kubaki kwenye timu kama Palace, ambayo kila msimu inakuwa inapambana isishuke daraja.

3.Harry Kane (Tottenham)

Kabla ya Mo Salah, straika Mwingereza, Harry Kane alibeba Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England mara mbili mfululizo, licha ya kuichezea Tottenham Hotspur, timu ambayo imeshindwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo.

Jambo hilo linaonyesha Kane alikuwa akifanya wajibu wake wa kufunga mabao, lakini shida ilikuwa kwa timu nzima kushindwa kulinda mabao hayo kushinda mechi.

Kane ni mchezaji anayekuhakikishia zaidi ya mabao 20 kila msimu na amefanya hivyo kwa zaidi ya misimu minne mfululizo.

Ni wazi si mchezaji wa kuendelea kuichezea Spurs, anapaswa kuwa kwenye klabu kubwa zaidi.

2.Neymar (PSG)

Paris Saint-Germain ililipa Pauni 198 milioni kunasa huduma yake, hilo pekee lilitosha kuthibitisha Neymar si mchezaji wa kawaida. Msimu wake wa kwanza alifunga mabao 28 na kuasisti 19 katika michuano yote aliyocheza na timu hiyo.

Lakini PSG haikufua dafu mbele ya Real Madrid ikichapwa kwenye hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ukweli Neymar hakustahili hilo, kwa sababu alipokuwa Barcelona alifikia mafanikio makubwa zaidi.

1.N’Golo Kante (Chelsea)

Kante alijigundua kuwa na uwezo wa juu sana alipokuwa Leicester City kuliko wachezaji wengine hapo walipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2016, hivyo akaamua kuondoa na kuhamia Chelsea.

Msimu uliofuatia akiwa na The Blues akabeba tena taji la ligi, mara ya pili mfululizo. Msimu huu Chelsea inacheza Europa League michuano ambayo kwa haki kabisa si kiwango cha Kante, kiungo huyo Mfaransa hapaswi kucheza huko, anga zake ni za juu zaidi.

Advertisement