Hakimu kesi ya Yanga mgonjwa

Muktasari:

  • Tangu kesi hiyo ilipofunguliwa wadaiwa hawakuwahi kufika mahakamani licha ya kupelekewa wito wa mahakama mara kadhaa na hata kutangazwa gazetini.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Aprili 29 kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi wa Klabu ya Yanga, upande mmoja bila wadaiwa kuwepo baada ya kushindwa kuitikia wito wa kufika mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa jana Jumatano katika mahakama hiyo, lakini iliahirishwa kutokana Hakimu anayesikiliza shauri, Janeth Mtega kuwa mgonjwa na hivyo kushindwa kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, ilifunguliwa, Januari 11, 2019, na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Juma A. Magoma na Athuman S. Nyumba dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika kesi hiyo, Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika uchanguzi huo kwa madai unakwenda kinyume cha Katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010, ibara ya 7.

Tangu kesi hiyo ilipofunguliwa wadaiwa hawakuwahi kufika mahakamani licha ya kupelekewa wito wa mahakama mara kadhaa na hata kutangazwa gazetini.

Kutokana na hali hiyo upande wa wadai kupitia Wakili wao Daudi Mzeri, Aprili 8 mwaka huu aliiomba mahakama hiyo iamuru kesi hiyo iendelee kusikilizwa upande mmoja, akidai imekuwa vigumu kwa mdaiwa huyo kuipokea hati ya wito iliyotolewa na mahakama.

Wakili Mzeri alidai kuwa licha ya Mahakama hiyo kuamuru, Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga kutangazwa katika gazeti la gazeti kama njia ya wito wa kufika mahakamani hapo, bado imekuwa vigumu kufika mahakamani hapo kusikiliza shauri hilo.

“Kutokana na wadaiwa wote kushindwa kufika mahakamani hapa licha ya mahakama kuamuru mdaiwa wa pili (Bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga) atangazwe gazetini lakini bado wameshindwa kufika mahakamani kusikiliza shauri lao.

“Hata Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) naye ameshindwa kufika mahakamani hapa,” alidai wakili Mzeri na kuongeza

“Kesi hii imetajwa mara tatu kwa maana ya Februari 11, Machi 11 na Aprili 8, bila wadaiwa kufika mahakamani kusikiliza shauri hili, hivyo kutokana na hali hii tunaiomba mahakama isikilize shauri hili upande mmoja,” alidai Mzeri.

Wakili Mzeri alidai kuwa mdaiwa wa pili katika shauri hilo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), alitangazwa Februari 8, 2019 kupitia gazeti, huku mdaiwa wa kwanza, yeye hajatangazwa gazetini kwa sababu alipokea wito wa mahakama, lakini hakufika mahakamani.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019, kwa lengo la kujaza nafasi mbalimbali zilizoachwa wazi, lakini ulishindikana kutokana na kufunguliwa kwa kesi hiyo.

Katika madai yao Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume cha katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.

Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambaye baaade yatajadiliwa na kamati tendaji. Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh.12,000 pamoja ana ada ya kadi ambayo ni Sh.2,000.

Pia wanadai kuna taarifa za kuwapo kwa wanachama wenye kadi feki za kieletroniki ambazo zina saini na mhuri ambazo zinasambaa kwa baadhi ya wanachama, ambazo zinaonyesha kuwa zimetolewa na benki ya CRDB pamoja na benki ya Posta.

Wanadai kadi hizo zinazodaiwa kuwa ni kadi za uanachama wa Klabu ya Yanga, zikiwa na picha za wamiliki ambazo sio mali ya klabu hiyo.

Hivyo wanapinga matumizi ya kadi hizo katika uchaguzi huo wakidai kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa uthibitisho wa uanachama wa Yanga, kwa kuzingatia kwamba, wahusika wa hizo kadi, hawakupitia utaratibu ulioanishwa katika ibara ya 7 ya mwaka 2010 ya klabu ya Yanga.

Wanachama hao wanapinga kumpa mtu uanachama bila kadi hiyo kusainiwa na kugong’wa mhuri wa klabu, hivyo haiwezi kutumika kuainisha uanachama wenye haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa klabu ya Yanga.