Hakimu ataka siku mbili za ushahidi kesi ya Aveva

Muktasari:

  • Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12 mwaka huu itakapotajwa na kuanza kusikilizwa ushahidi Februari 18 na 19.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka umetakiwa kuwaanda mashahidi watatu watakaotoa ushahidi kwa siku mbili mfululizo katika kesi inayowakabili aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe.

Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba alitoa amri hiyo baada ya shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Boaz Mbupira kukamilisha kutoa ushahidi wake alioanza kuutoa tangu Oktoba 2018.

"Tunataka shauri hili liishe kwa haraka na ninatalisikilizwe kwa mfululizo hivyo nawataka Waendesha mashtaka muwaandae  mashahidi watatu  ambao watatoa ushahidi wao kwa siku mbili mfululizo ,"alisema Hakimu Simba.

Shahidi Mbupira afisa wa CRDB tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam alitoa ushahidi wake katika kesi hiyo kuhusiana na kielelezo cha taarifa fupi ya kifedha (Bank statement), iliyopokewa mahakamani hapo kama kielelezo cha usahahidi wa upande wa mashtaka.

Katika ushahidi wake, shahidi huyo akiongozwa na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai, alidai kuwa mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kutoka Simba kwenda klabu ya Etoile Du Sahel kwenye akaunti namba 02J1026761800 ambazo zilikuwa ni dola 319, 212.

"Kiasi kilichoingizwa kwenye akaunti namba 02J1026761800 na maelezo ya Bank Statement (Taarifa fupi ya akaunti) ndiyo maelekezo unayoyapata kwenye swift Message,” alidai.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12 mwaka huu itakapotajwa na kuanza kusikilizwa ushahidi Februari 18 na 19 mwaka huu.

Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo yeye pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakayishaji fedha yanayowakabili wote, Aveva na Kaburu.

Katika maelezo ya awali, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Machi 12, 2016, Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia.

Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia.