Habibu Kiyombo kupigwa msasa kwanza

Muktasari:

Mmoja wa mawakala wa kituo hicho, Ibrahim Mohamed aliliambia Mwanaspoti kuwa mawazo yao watayawasilisha kwenye uongozi wa klabu ya Mamelod ambao watajadiliana kama watakubali kupelekwa kwa mkopo ama kubaki naye hapo.

MAWAKALA wa straika Habibu Kiyombo huenda wakampeleka mchezaji huyo timu nyingine kwa mkopo ili kulinda kiwango chake kabla hajaanza rasmi kugombea namba katika kikosi cha Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini iliyomsajili hivi karibuni.
Kiyombo yupo chini ya kampuni ya Shadaka inayosimamia wachezaji mbalimbali wanafikiria kufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa ni kuzoea soka la huko.
Mmoja wa mawakala wa kituo hicho, Ibrahim Mohamed aliliambia Mwanaspoti kuwa mawazo yao watayawasilisha kwenye uongozi wa klabu ya Mamelod ambao watajadiliana kama watakubali kupelekwa kwa mkopo ama kubaki naye hapo.
Alisema lengo ni kupata muda wa kucheza kwani akibaki ndani ya kikosi hicho hatapata nafasi kirahisi ya kucheza kwa vile ligi ni tofauti.
"Bado yupo ndani ya Mamelod hadi sasa, sisi ndiyo tunafikiria kumtafutia timu nchini humo ambayo atapata nafasi ya kucheza ili kuzoea soka la huko japo kwa miezi sita ndipo aingie kupambania namba Mamelod.
"Mawazo yetu bado hatajawasilisha Mamelod ila nadhani tutayawasilisha na kuwasikiliza wao kama watakubali basi atakwenda kucheza kwa mkopo, wakigoma atabaki hapo hapo.
"Kiyombo ametoka kwenye ligi tofauti na ya kule, hivyo kuingia moja kwa moja kikosi si rahisi sana, na kwa kuona hivyo ndiyo maana tumefikiria kumtafutia timu kwa mkopo ili kulinda kipaji na kuzoea ligi," alisema Mohamed
Mamelod Sundowns walimsajili Kiyombo akitokea Singida United ambako alikuwa kinara wa mabao pia aliichezea Mbao FC ya Mwanza.