Haaland kinda mchana nyavu anayesakwa Ulaya

Muktasari:

Kipaji chake cha kupachika mabao kimezikuna klabu nyingi kubwa Ulaya na anaonekana hakamatiki. Ni nani Erling Haaland?

LEIPZIG, AUSTRIA . KAMA kuna kinda anayewindwa zaidi Ulaya kwa sasa basi ni huyu wa RB Salzburg ya Austria, Erling Haaland.

Kipaji chake cha kupachika mabao kimezikuna klabu nyingi kubwa Ulaya na anaonekana hakamatiki. Ni nani Erling Haaland?

Azaliwa England, mtoto wa staa

Jina lake kamili ni Erling Braut Haland na alizaliwa Julai 21, 2000 katika Jiji la Leeds nchini England, wakati huo baba yake, Alf Inge Haland akiwa staa mkubwa wa Leeds United. Baba yake pia amewahi kutesa na klabu za Manchester City na Nottingham Forest.

Haland ni shabiki mkubwa wa Leeds licha ya kwamba alirudi kwao Norway na baba yake akiwa na umri wa miaka mitatu tu. Amewahi kukaririwa akidai moja kati ya ndoto zake ni kucheza Leeds United.

Baada ya kurudi kwao katika mji wa Bryne alianza kucheza soka katika klabu ya Bryne FK. Msimu wa 2015–16, Håland alicheza timu ya wachezaji wa akiba ya Bryne FK 2 akifunga mabao 18 katika mechi 14.

Kiwango chake kilisababishe aitwe katika kikosi cha wakubwa akiwa na umri wa miaka 15 tu. alicheza mechi yake ya kwanza Mei 12, 2016 dhidi ya Ranheim. Wakati akiwa na Bryne alifanya majaribio na klabu ya TSG 1899 Hoffenheim ya Ligi Kuu ya Ujerumani bila ya mafanikio. Haland alicheza mechi 16 kwa Bryne.

Atinga Molde, anolewa na Ole 

Februari Mosi 2017, klabu maarufu ya Norway ya Molde FK ilitangaza kumnasa Erling Braut Haland. Alicheza mechi yake ya kwanza April 26, 2017 katika pambano la kombe la Norway dhidi ya Volda TI. Alifunga bao lake la kwanza kwa Molde katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Volda. Mechi yake ya kwanza ya Ligi ilikuja Juni 4, 2017 akitokea benchi dakika ya 71 dhidi ya Sarpsborg 08. Alipewa kadi ya njano sekunde 65 tu tangu aingie. Dakika ya 77 akafunga bao lake la kwanza katika Ligi hiyo.

Bao lake la pili lilikuja Septemba 17 akifunga bao la ushindi dhidi ya Viking katika matokeo ya 3-2. Hata hivyo, alikosolewa vikali kwa kushangilia bao hilo mbele ya mashabiki wa Viking. Alimaliza msimu akiwa mabao manne katika mechi 20.

Afunga mabao manne dakika 21

Msimu uliofuata mnamo Julai Mosi, 2018, Haland alifunga mabao manne ndani ya dakika 21 za pambano dhidi ya Brann ugenini. Mabao matatu alifunga ndani ya dakika 11 na sekunde mbili wakati mabao yote manne alifunga dakika 17 na sekunde nne.

Katika pambano hilo skauti wa Manchester United alikuwepo uwanjani. Kocha wa Molde FK, Ole Gunnar Solskjaer aliilinganisha staili ya Haland na ile ya Romelu Lukaku huku akitoa siri kuwa, klabu yake ilikuwa imekataa ofa kibao za kumuuza staa huyo.

Mechi iliyofuata mnamo Julai 8, Haland aliendeleza fomu yake ya kufunga mabao akifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Vålerenga. Akafunga pambano la michuano ya Europa dhidi ya KF Laçi katika ushindi wa mabao 3–0 Julai 26.

Baadae aliumia kifundo cha mguu na kukosa mechi tatu za mwisho za Molde. Hata hivyo, mwishoni mwa msimu akapewa tuzo ya kinda bora wa Ligi Kuu ya Norway. Alimaliza msimu wa 2018 akiwa na mabao 16 katika mechi 30 za michuano mbalimbali na kuwa mfungaji bora wa klabu.

Salzburg yamnasa, atesa

Agosti 19, 2018 klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria ilitangaza kumnasa Haland kwa mkataba wa miaka mitano akijiunga na timu hiyo Januari Mosi 2019. Julai 19, 2019 alipiga Hat trick yake ya kwanza katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya SC-ESV Parndorf kombe la Austria.

Akapiga hat trick yake ya kwanza Ligi Kuu Agosti 10 katika ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Wolfsberger AC. Akapiga Hat trick yake ya tatu Septemba 14 katika ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya TSV Hartberg, akiweka rekodi ya kufunga mabao 11 katika mechi saba tu.

Avunja rekodi kibao za Ulaya

Siku tatu baadaye akapiga hat trick nyingine katika ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Genk michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Alifikisha mabao manne. Akafunga tena bao moja dhidi ya Liverpool na mawili dhidi ya Napoli.

Kwa kufanya hivyo alikuwa kinda wa pili nyuma ya Karim Benzema kufunga katika mechi zote tatu za kwanza katika michuano hiyo. Lakini, alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kufunga mabao sita katika mechi zake tatu za kwanza. Akafunga tena dhidi ya Napoli na hivyo kuwa kinda wa kwanza kufunga katika mechi nne mfululizo za Ligi ya Mabingwa. Pia, akawa mchezaji wanne kwa ujumla kufanya hivyo akifuata rekodi za Zé Carlos, Alessandro Del Piero na Diego Costa. Novemba 27, Jumatano iliyopita akafunga bao jingine dhidi ya Genk na hivyo, kufikia rekodi ya kufunga mechi tano mfululizo. Alifikia rekodi iliyowekwa na akina Alessandro Del Piero, Serhiy Rebrov, Neymar na Robert Lewandowski waliowahi kufanya hivyo.

Aitosa England

Kutokana na kuzaliwa Leeds, Haland alikuwa na uwezo wa kucheza timu ya taifa ya England, lakini kwa sababu alirudi kwao akiwa na umri wa miaka mitatu aliamua kuiwakilisha Norway katika ngazi za vijana hadi sasa timu ya wakubwa. Akiwa na kikosi cha Norway chini ya umri wa miaka 19 alipiga hat trick katika pambano dhidi ya Scotland waliloshinda 5-4 na kufuzu michuano ta Euro chini ya umri wa miaka 19. Julai 22, 2018 akaifungia Norway katika sare ya 1-1 dhidi ya Italia katika michuano ya Euro 2018 chini ya miaka 19.

Apiga bao tisa mechi moja

Mei 30, 2019 Haland alifunga mabao tisa katika pambano la chini ya umri wa miaka 20 kati ya Norway dhidi ya Honduras huku Norway wakishinda mabao 12-0 katika michuano ya kombe la dunia chini ya umri wa miaka 20 jijini Lublin nchini Poland.

Mechi hiyo iliweka rekodi ya mabao mengi zaidi kufungwa na mchezaji mmoja huku pia ikiweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi dhidi ya timu nyingine. Licha ya Norway kutolewa hatua ya makundi huku Haland akishindwa kufunga tena, bado alitwaa kiatu cha dhahabu.

Baada ya kung’ara katika michuano hiyo ya kombe la dunia chini ya umri wa miaka 20, huku pia aking’ara klabuni kwake, Agosti 28 kocha wa timu ya taifa ya Norway, Lars Lagerback alimuita katika kikosi cha wakubwa kwa ajili ya mechi za kufuzu 2020 Euro dhidi ya Malta na Sweden na alicheza mechi yake ya kwanza Septemba 5, 2019.