HISIA ZANGU : Musonye na michuano yake ya kisela tu!

Wednesday June 12 2019

 

By Edo Kumwembe

“Yanga ni timu isiyo na lolote na wala hatutawamiss. Hawakushiriki michuano iliyopita na kumbuka kwamba, wao sio mabingwa wa Tanzania. Hatutawamiss na acha waende zao. Haishangazi kuona katika michuano ya Caf siku zote wanafungwa 5-0 au 6-0. Wala hatujali kujitokea kwao.”

Anazungumza hayo mtu anayeitwa Nicholas Musonye. Nadhani alikuwa amekasirika. Huyu ni katibu mkuu wa Cecafa. Anaonekana kuwa na hasira kwa kujitoa kwa klabu mbili za Simba na Yanga katika michuano yake ya kipuuzi.

Yanga walikuwa wamealikwa tu katika michuano hii. Ni yeye ndiye ambaye amewaalika. Kwa nini kujitoa kwao kunamkasirisha na kudai kwamba, ‘hatawamiss?” Ni kama vile unamuita nyumbani mpenzi wako na anaposema hawezi kuja unadai kwamba ‘hautammiss’. Ajabu iliyoje. Kwa nini ulimuita kama haumpendi?

Achilia kila kitu lakini ugomvi wa Musonye na Yanga ulianza pale wakati Yanga walipogoma kuingiza timu kwenye pambano la mshindi wa tatu dhidi ya Simba miaka kadhaa iliyopita na Musonye akakosa pesa nyingi za kulipia madeni ya Cecafa kwa timu alizozileta nchini.

Zamani kabla ya Musonye michuano hii ilikuwa dili kubwa kwa Simba na Yanga na mashabiki wao. Siku hizi sio ajabu kwa klabu hizi kujitoa kwa sababu ni michuano ambayo haieleweki. Inaendeshwa kwa ujanja ujanja tu.

Mwaka jana Yanga walijitoa, Simba wakatamba sana. Mwaka huu wameanza kujitoa Simba lakini Yanga wakakaa kimya. Sababu ni rahisi tu. Yanga walishajua ujinga wa michuano yenyewe kabla ya Simba. Na walijua kwamba hata wao wenyewe wapo safarini kujitoa.

Advertisement

Musonye huwa anachungulia tu. Hajui ni lini michuano yake huwa inafanyika. Hana kalenda maalumu. Mara kadhaa michuano yake imeshindwa kufanyika kwa kukosa mdhamini au kwa nchi nyingi kugoma kuandaa.

Anapoona mambo mazito basi anaikimbizia michuano hii Dar es Salaam. Kisa? Kuna Simba na Yanga. Anajua Watanzania wanapenda sana soka. Anataka Simba na Yanga ziiingizie viingilio ambavyo vitaweza kulea michuano yenyewe kwa mwaka husika.

Akiona watu wa Dar es Salaam hawataki michuano, anaipeleka Kigali kwa Rais Paul Kagame. Ni kwa sababu Kagame anapenda soka na ndiye mdhamini wa michuano yenyewe. Kule anapewa msaada ulio nje ya utaratibu kwa ajili ya kufanikisha. Ni michuano ya kisela tu.

Kwa mfano, michuano yake ya mwaka huu inaanza Julai 7 mpaka Julai 21. Wakati huohuo dunia itakuwa bize na michuano ya Afcon ambayo itaanza Juni 21 mpaka Julai 21. Simba na Yanga zina wachezaji wake muhimu wanaoshiriki Afcon kutoka katika nchi za ukanda huu.

Alichotazama Musonye ni kujidharau mwenyewe. Anaamini kwamba mpaka kufikia Julai 7, timu zote za ukanda huu ambazo zinashiriki Afcon, Kenya, Tanzania, Burundi na Uganda zitakuwa zimetolewa katika michuano hiyo na wachezaji wake watawahi katika michuano yake. Katibu wa Cecafa haamini kwamba timu za ukanda wake zitafanya chochote katika michuano hiyo. Ajabu iliyoje. Anadharau watoto wake.

Lakini kumbuka kwamba hii ni mchuano iliyokuwa na hadhi hapo awali. Watu wanataka kwenda pale kushinda taji na sio kucheka. Julai 7 au 8, au 8, au 10 ni nyakati ambazo michuano mikubwa huwa inamalizika sio kuanza. Kombe la Dunia, Mataifa ya Afrika, Mataifa ya Ulaya (Euro) na mengineyo. Hata Copa Amerika ambayo inafanyika mwaka huu itamalizika Julai 7.

Kwa nini michuano inamalizika tarehe hizo na sio kuanza? Kwa sababu wachezaji inabidi wakapumzike, au waanze mazoezi kwa ajili ya msimu ujao, ambao kwa mujibu wa kalenda ya Fifa duniani kote, ligi huwa zinaanza Agosti.

Wakati michuano mikubwa ikimalizika tarehe hizo, Musonye anaanzisha michuano tarehe hizo. Tarehe ambazo hata wachezaji waliokwenda Afcon Misri wanahitaji kuwa mapumzikoni. Wale ambao hawakwenda katika michuano hii wanapaswa kuanza mazoezi mepesi na timu zao. Musonye anachomekea michuano tarehe hizo.

Hapo hapo tukumbuke kwamba michuano hii haijawahi kupata wadhamini. Inadhaminiwa na Rais Paul Kagame, ambaye huwa anazipatia timu zawadi tu. Mshindi anachukua Dola 30,000 na haijawahi kubadilika.

Ni michuano isiyokua. Imedumaa. Musonye huwa anaonekana katika michuano hii tu baada ya hapo anapotea. Jina lake ni maarufu kwa michuano hii, lakini kama haipo hauwezi kusikia akihusishwa tena na timu za ukanda huu. Umewahi kusikia Cecafa inazitakia heri Simba na Yanga katika michuano yake ya kimataifa?

Umewahi kusikia Cecafa imetoa kiasi fulani cha pesa kwa Simba na Yanga ili zijiandae vyema na michuano ya kimataifa ya Caf? Hauwezi kusikia. Musonye anaishi kwa ajili ya michuano hii tu. Hata anapokuja Dar es Salaam huwa anakuja kwa ajili ya michuano hii.

Kama Musonye anataka kurudisha hadhi ya michuano hii basi aache ujanja ujanja. Atafute mfumo mpya, wadhamini wapya.

Kwa sasa Simba na Yanga zina baadhi ya watu walioelimika zaidi tofauti na wale ambao alizoea kuwaburuta huko nyuma.

Advertisement