HISIA ZANGU : Tusiisahau kesi hii ya Zaha na Man United

Muktasari:

Kwa kutumia akili hii, leo United wanaweza kupata asilimia 25 ya mauzo ya Zaha ambaye ameibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri katika kikosi cha Palace na Ligi Kuu ya England kwa jumla. Arsenal wanamtaka Zaha.

NI nyakati sahihi zaidi ya kuwakumbusha waendesha soka letu jinsi pesa ya uhamisho ilivyo tamu kuliko pesa ya ubingwa. Nawaletea kesi ya mchezaji anayeitwa Wilfried Zaha. Anacheza Crystal Palace. Nadhani wengi tunamfahamu.

Ni mchezaji wa mwisho kununuliwa na Sir Alex Ferguson pale Manchester United ingawa hakuwahi kufundishwa na kocha huyu Mscotland. Alinunuliwa Januari 2013 kutoka Crystal Palace kisha akaachwa hapo hapo kwa mkopo mpaka mwishoni mwa msimu.

Bahati mbaya, Sir Alex akaondoka Mei 2013. Akastaafu kufundisha soka. Akawa amepishana na mchezaji aliyemnunua mwenyewe. Kuna sababu ambazo zilimfanya

amnunue Zaha. Alijua kwamba siku za usoni angekuwa tishio Old Trafford.

Hata hivyo, kocha aliyekuja, David Moyes hakukiona kitu ambacho Sir Alex alikiona kwa Zaha. Akaamua kumtoa kwa mkopo Cardiff City. Baadaye akamtoa kwa mkopo tena, Crystal Palace ambayo ilikuwa timu iliyomuuza Zaha kwenda United.

Mwaka 2015 wakamuuza Zaha jumla. Hata hivyo, kitu cha msingi zaidi ambacho hatufanyi katika soka ni hiki ambacho United walifanya. Waliweka kipengele cha kwamba siku ambayo Palace wakimuuza Zaha kwenda kwingine basi watalazimika kulipwa kiasi cha asilimia 25 za mauzo.

Kwanini waliweka kiasi hiki? Sababu ni rahisi. Wazungu wa Old Trafford walijua Sir Alex sio mjinga. Walijua kuna kitu alikiona kwa Zaha na siku moja Zaha anaweza kukitumia vyema kipaji chake kwingineko.

Walijua inawezekana Moyes hakuona kitu kwa Zaha na wakaheshimu mawazo yake, lakini kwa wakatumia mawazo yaleyale ya Sir Alex kupenyeza kipengele hiki. Walijua huenda kuna siku huyu mtu akaibuka kuwa staa mkubwa duniani.

Kwanini walifanya hivi? Wenzetu kocha huwa anapewa uamuzi mkubwa lakini pia kuna watu wengi ambao, wameajiriwa na klabu kwa ajili ya kuangalia ujumla wa viwango vya wachezaji kabla ya kutua klabuni na wakati wanaondoka klabuni.

Kuna makocha wengi kama Moyes ambao waliwahi kufanya makosa huko nyuma. Na ndio maana wazungu wameamua kuja na mfumo ambao utamfanya kocha awe sehemu ya uamuzi. Ni wazi kwamba kuna baadhi yao hawakumuamini sana Moyes na ndio maana waliingiza kipengele hiki kwa ajili ya kuhakikisha wanaweza kupata pesa kama mchezaji akija kutumia kipaji chake vema siku za usoni.

Kwa kutumia akili hii, leo United wanaweza kupata asilimia 25 ya mauzo ya Zaha ambaye ameibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri katika kikosi cha Palace na Ligi Kuu ya England kwa jumla. Arsenal wanamtaka Zaha. Wanapambana kumnasa Zaha. Palace wanataka kumuuza lakini kikwazo kikubwa kinakuja katika kile kipengele ambacho waliingia na United.

Palace wanataka kumuuza Zaha kwa dau la Pauni 80 milioni. Sio thamani hasa ya Zaha, lakini inabidi wafanye hivyo ili waambulie Pauni 60 milioni. Pauni 20 milioni itakwenda kwa Manchester United. Kumbuka United wanaisubiri pesa hii wakati wao walimnunua Zaha kwa dau la Pauni 10 milioni tu Januari 2013.

Endapo Palace watalazimika kumuuza Zaha kwa dau la Pauni 60 milioni basi United wataambulia Pauni 15 milioni. Sio neno kwao. Kitu cha msingi ni kwamba United walitabiri Zaha anaweza kuibuka tena muda wowote kama akitulia au akitulizwa mahala.

Mfano huu hapa kwetu una maana mbili. Kwanza kabisa kuna wachezaji ambao unahisi wanaweza kuibuka tena siku za mbele licha ya kutofanya vema klabuni kwa wakati husika. Hakuna haja ya kuwa na tamaa ya kuwauza kwa pesa nyingi. Kitu cha msingi ni kuweka kipengele hiki ambacho United wameweka.

Lakini, pia kuna wachezaji ambao wamefanya vema klabuni lakini wanahitajika kwingine. Hakuna haja ya kuwauza kwa bei ghali kama ambavyo mabosi wa klabu zetu huwa wanaropoka na wakati mwingine wanaharibu maisha ya wachezaji.

Kitu cha msingi ni kuingiza kipengele hiki ambacho United wameingiza kwa Zaha. Ni muhimu. Kwa mfano, Yanga wamemuuza Heritier Makambo kwenda Horoya ya Guinea. Wameingiza kipengele hiki? Makambo ana miaka 25 tu, vipi akiwasha moto na baada ya miaka miwili akanunuliwa na Al Ahly kwa Dola 1.2 milioni?

Kuna huyu Adam Salamba. Anaonekana hafai kwa sasa, lakini Simba sio wajinga kumchukua kutoka Lipuli. Kuna kitu walikiona. Iweje amechemka ghafla? Labda anahitaji kutulia. Vipi kama akipata utulivu akarudi katika fomu ya hali ya juu?

Simba wanahitaji kumuongezea mkataba kisha wakamuuza kwenda sehemu nyingine kwa bei ndogo lakini wakaingiza kipengele hiki. Inaweza kuwa ndani au nje. Vipi akibaki nchini na kufunga mabao mengi kisha akatamaniwa na Yanga au Azam? Simba inaweza kuambulia chochote.

Kuna wachezaji wengi waliokwenda klabu ndogo, wakaibuka imara, wakarudi katika klabu kubwa. Manchester ilijua tu kwamba kile alichokiona Sir Alex kwa Zaha kinaweza kuibuka tena na akatamaniwa na klabu kama Arsenal, Manchester City, Liverpool au Chelsea.

Ndicho kinachotokea kwenye dunia ya sasa ya soka lenye watu werevu.