HISIA ZANGU : Namuona Zahera mlango wa ‘Exit’

Muktasari:

Msimu huu Yanga wamejipanga kidogo. Wamechagua uongozi wao, kwa hiyo wamemuondolea ‘uenyekiti’ aliojipa pamoja na kazi nyingine. Na sasa analazimika kurudi katika kazi iliyomleta klabuni. Na sasa ataanza kuhukumiwa zaidi kwa kazi hiyo iliyomleta.

RAFIKI yangu Mwinyi Zahera msimu uliopita alikuwa na kazi nyingi pale Yanga. Alikuwa mwenyekiti, mfadhili, msemaji wa timu, mweka hazina na pia kocha. Alifanya kila kazi. Wakati mwingine ungeweza kuwashangaa Yanga. Uvumilivu ule walikuwa wameutoa wapi?

Haikuwahi kutokea katika maisha ya Yanga, licha ya timu yao kuwahi kufundishwa na makocha wakubwa, lakini haikuwahi kutokea kocha akageuka kuwa rais wa klabu. Nadhani hata mwenyewe Zahera haijawahi kutokea akaongoza umati mkubwa wa watu kama alivyogeuka kuiongoza Yanga ndani na nje ya uwanja huku akiwa kocha tu.

Msimu huu Yanga wamempunguzia kazi zote. Wamemuachia kazi yake ya ukocha tu. Msimu uliopita hata kama angefeli katika kazi ya ukocha bado walimuhitaji katika kazi nyingine kama vile kutembeza bakuli. Wakati mwingine alikuwa anatoa pesa zake za mfukoni kusaidia timu.

Msimu huu Yanga wamejipanga kidogo. Wamechagua uongozi wao, kwa hiyo wamemuondolea ‘uenyekiti’ aliojipa pamoja na kazi nyingine. Na sasa analazimika kurudi katika kazi iliyomleta klabuni. Na sasa ataanza kuhukumiwa zaidi kwa kazi hiyo iliyomleta.

Hii ni kazi ngumu zaidi kuliko nyingi katika nchi hii. Achana na kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Waziri Mkuu ama Waziri wa Fedha, moja kati ya kazi ngumu nchi hii ni kuwa mwenyekiti wa Simba na Yanga au kocha wa klabu hizi mbili za Kariakoo.

Niliwatazama Yanga msimu uliopita. Kasoro mechi ya marudiano dhidi ya Simba, lakini mechi nyingi hawakunifurahisha. Waliposhinda, walipotoka sare, walipofungwa bado walionekana kuwa timu ya kawaida. Hawakumiliki mpira vyema wala hawakucheza kimamlaka kuonyesha kwamba wao walikuwa timu kubwa.

Mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya watani wao Simba inaingia katika historia kama mechi ya upande mmoja zaidi katika historia ya watani hawa. Nadhani Simba walipiga mashuti zaidi ya 30 yaliyotoka nje au kulenga lango la Beno Kakolanya.

Haya yote mashabiki walimezea baada ya kujua kwamba kocha wao alikuwa na kazi nyingi klabuni. Walimhitaji. Na ni kweli kwamba kocha alijua kuwateka. Alijua kufanya kazi nyingi zisizomhusu na mashabiki na wanachama wakaamini kwamba kocha alikuwa mnazi asiyestahili kufukuzwa.

Zaidi ya yote ni kwamba Yanga wenyewe walifahamu kwamba hawakuwa na timu nzuri. Walikuwa na wachezaji wawili watatu ambao wangeweza kuonyesha maajabu ya ghafla. Herritier Makambo, Ibrahim Ajib na Fei Toto waliongoza kundi hili la kutoa maajabu ya ghafla ghafla. Vinginevyo Yanga walikuwa timu ya kawaida tu.

Msimu huu Yanga wanajiamini kwamba wana timu. Wanajiamini kwamba wana wachezaji wa maana. Ndio maana walipotoka sare katika pambano dhidi ya Township Rollers ya Botswana mashabiki wameanza kuguna chini chini.

Majuzi walikuwa wakicheza mechi ya kirafiki pale Moshi wakafungwa mabao 2-0, mashabiki wameendelea kuguna. Juzi wakashinda dhidi ya AFC Leopards, mashabiki wamehema kidogo. Yanga ikitolewa na Rollers katika mechi ya marudiano naweza kusikia miguno yao ikienda juu zaidi.

Nawafahamu Yanga. Naelewa simile yao kwa kocha wao msimu uliopita. Lakini msimu huu sidhani kama watamuelewa. Bakuli lao linaendeshwa kisayansi kidogo msimu huu na sidhani kama wanamuhitaji sana Zahera katika upande huo. Wanamuhitaji katika upande wa uwanjani.

Simba na Yanga zina tabia moja. Zikijiridhisha kwamba zimesajili vizuri halafu matokeo yasiwe mazuri basi mashabiki wanaanza kunong’onezana “uwezo wa kocha umefika mwisho”. Mwingine anasema “wachezaji wamemzidi kocha uwezo”. Ukiona hivyo ujue tayari paka amevalishwa kengele.

Njia pekee kwa sasa ya Zahera kuendelea kupendwa na kuaminiwa ni Yanga kuitoa Rollers ugenini. Kama ikitolewa basi safari yake itaanza kuiva. Yanga na Simba wanapotolewa mapema katika michuano hii, huku wakiamini wana timu nzuri, kuna mazingira ya kuondoka kwa kocha yanakaribishwa.

Kitu kingine ambacho kitamponza zaidi Zahera ni kwamba watani wao wamerudi na motomoto uleule. Yanga na Simba wana tabia ya kutojali mchakato wa uvumilivu. Ghafla Yanga watataka timu yao icheze kama Simba au zaidi ya Simba bila ya kujali kwamba Simba ilishakuwa katika hatua kadhaa mbele ikiwemo kucheza robo fainali ya michuano ya Afrika.

Yanga wangeweza kuendelea kuridhika kuwa na Zahera kama Simba ingerudi ikiwa mbovu msimu huu, lakini kwa kadri ninavyowaona Simba wanavyocheza nadhani wataendelea kumchongea Zahera kila siku. Ndio maisha yao waliyojichagulia. Kuchunguliana. Wafaransa wanaita voyeur.

Vyovyote ilivyo, namuona Zahera ameshika kitasa katika mlango ulioandikwa Exit. Mlango wa kutokea. Msimu huu anaweza kuelewa zaidi kwanini Yanga inaitwa timu ya wananchi. Lakini pia atajua tabia halisi ya watu wa Yanga. Nadhani msimu uliopita umaskini wao ulimsaidia kwa kiasi kikubwa.

Huu ndio msimu ambao hawatamuelewa kwa maamuzi kama yale aliyochukua kwa Beno Kakolanya na kumuweka Klause Kindoki katika lango huku msaidizi wake akiwa kinda, Ramadhan Kabwili. Hata huyu mshambuliaji aliyemleta anaweza kuwa chanzo cha yeye kuondoka.