HISIA ZANGU : Kwanini tuwazuie Yondani na Erasto kustaafu?

Tuesday July 16 2019

 

By Edo Kumwembe

INACHEKESHA lakini ndio hali halisi. Hatutaki Kelvin Yondani na Erasto Nyoni wastaafu katika kikosi cha timu ya taifa. Kwa mujibu wa Wikipedia, Yondani ana umri wa miaka 34. Erasto Nyoni ana umri wa miaka 31.

Wana mwenzao anaitwa Aggrey Morris ana miaka 35. Aggrey ni jembe kwelikweli. Mti mkavu. Mmoja kati ya wachezaji ambao tuliwakosa katika michuano hii baada ya kuumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeweji Misri.

Aggrey hajatangaza kustaafu, lakini katika hawa watatu yeye ndiye aliyepaswa kuwa wa kwanza kustaafu. Hata hivyo, tuwajadili kidogo hawa ambao wametangaza kustaafu na bado mioyo yetu imegoma kuwaona wakistaafu.

Tuseme hawakudanyanya miaka yao. Tuiache kama ilivyo. Bado wanaweza kuwa na hoja nyingi za kustaafu. Miaka miwili ijayo kama Stars itakwenda Afcon, basi Yondani atakuwa na miaka 36 wakati Erasto atakuwa na miaka 33.

Kwanini hatutaki wastaafu? Sisi sio wajinga. Tunajua hatuoni wabadala wao. Akishastaafu Yondani halafu pale nyuma acheze nani? Na vipi tunaiachaje akili ya Erasto nje ya uwanja? Kuna mchezaji anayetumia akili zaidi yake?

Hatuoni wabadala wao. Tatizo kubwa ni kwamba sio kwamba hatuoni wabadala. Tatizo ni kwamba hatuoni kosa. Kosa letu lilikuwa wapi? Kosa letu kubwa na la msingi ni kwamba wachezaji wetu wanachelewa sana kupevuka.

Advertisement

Yondani na Nyoni wenyewe tulikuwa nao kwa miaka mingi, lakini wameanza kuja kuwa ‘watamu’ wakati miaka ikiwa imekatika. Ubora wa wachezaji wa Tanzania unachelewa kuja. Wachezaji wanakusanya uzoefu kwa miaka mingi halafu ndio wanapevuka wakati taifa linawahitaji.

Ukweli ni kwamba Yondani na Nyoni ni wazee kwa mujibu wa taratibu za soka na inabidi wapishe wachezaji wengine. Hawa wachezaji wengine ambao wanaweza kupishwa bado hawajapevuka ingawa nao wana umri mkubwa.

Muundo wetu wa soka ni hafifu. Wachezaji wetu vijana hawachezi mechi nyingi na wala hawafiki madaraja ya juu kwa haraka. Wanachelewa chini. Yondani na Nyoni wamewekeza uzoefu wao kwa miaka mingi na sasa tunawahitaji angali wakiwa wazee.

Kwa wenzetu hali ni tofauti. Mtazame mchezaji kama Aaron Wan-Bissaka. Amenunuliwa Pauni 50 milioni na Manchester United akiwa na umri wa miaka 21 na mpaka United inatoa pesa hizo bado hajagusa katika Timu ya Taifa ya England.

Hata hivyo, soka la kwao England limemkomaza kwa sababu ya muundo wake. Amecheza mechi nyingi katika timu ya vijana ya Crystal Palace, lakini pia amecheza mechi nyingi za Timu ya Taifa ya England chini ya umri wa miaka 17, kisha chini ya umri wa miaka 19 na sasa yupo kikosi cha England chini ya umri wa miaka 21.

Huko kote amekusanya uzoefu wa kutosha na sasa ana miaka 21 tu, lakini amekomaa kimwili na kiakili. Hapa ndipo lililpo tatizo la mfumo wetu. Kina Yondani na Nyoni hawakucheza sana katika timu za vijana na uzoefu wameupatia humo katika timu za wakubwa. Na sasa tuna hofu na wale wanaotaka kupatia uzoefu katika timu za wakubwa.

Tulipaswa kuwa na mfumo imara wa soka na lishe kwa wachezaji chipukizi ndani ya klabu zetu na pia kwa wadau wakubwa wa soka TFF kwa wale wachezaji wenye vipaji. Wafaransa wana kambi yao inayoitwa Clairefontaine ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka la Ufaransa.

Wachezaji wetu wana miili midogo na wanachelewa kupevuka. Ukienda katika klabu zetu za vijana unakutana na vijeba ambao ni wazi wana miaka 24 hadi 26. Katika karatasi tunasema wana miaka 17. Hilo bado sio tatizo. Tatizo ni kwamba hata katika umri huo ambao wamedanganya bado wanakuwa hawajapevuka.

Tazama kikosi cha Serengeti Boys ambacho kilikwenda Gabon miaka mitatu iliyopita. Kina Yohana Mkomola walipoingia katika vikosi vya Ligi Kuu walikuwa bado hawajapevuka kimwili wala kiakili. Mkomola pale Yanga alionekana kama mtoto tu wakati alipaswa kuwa Wan-Bissaka. Alipaswa kuingia katika timu na kuaminiwa.

Ukimtazama Kabwili naye ni hivihivi. Anaonekana mtoto. Ana miaka 18. Tatizo sio umri wake. Tatizo ni mwili wake, akili yake na hata uwezo wake uwanjani. Bado inaonekana hawezi kuhimili mikiki. Lakini kipa namba moja wa AC Milan na Timu ya Taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma ana miaka 20. Ni tegemeo la Waitaliano wote.

Wamepishana miaka miwili tu na Kabwili, lakini itamchukua Kabwili miaka 10 kuja kuwa kipa tegemeo wa Taifa Stars wakati Donnarumma ameanza kuwa kipa namba moja wa Italia miaka miwili iliyopita akiwa na umri wa Kabwili.

Tunahitaji kuwa na mfumo sahihi wa vijana. Mfumo ambao unazingatia malezi mazuri likiwemo suala la lishe. Baada ya hapo vijana wawe na michuano mingi ndani na nje ya nchi. Wakomae mapema na wadakwe na timu kubwa wakiwa na umri mdogo huku wakiwa tegemeo katika timu hizo.

Advertisement