HISIA ZANGU : Juma kaseja wa miaka 19 baadae

Muktasari:

Ana hamu ya kuendelea kukaa langoni. Matokeo yake anabakia kuwa mchezaji anayetajwa kufanya mazoezi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini.

NILIANDIKA hapa, siku si nyingi, Kelvin John alikuwa hajazaliwa wakati Juma Kaseja Juma alipokuwa langoni Cairo wakati Simba ikicheza dhidi ya Zamalek na kutinga robo fainali ya michuano ya Afrika. Miaka 19 iliyopita. Nyakati zimekwenda wapi?

Ilikuwa ni katika utawala wa Rais wa awamu ya tatu, Ben Mkapa. Ukaja utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete. Sasa tupo katika utawala mwingine. Kaseja yupo langoni. Ana hamu ya kucheza. Kila siku anataka kucheza.

Juzi katika pambano dhidi ya Burundi ametuokoa kwa mara nyingine. Linapofika suala la penalti Kaseja anakwenda langoni akiamini anakwenda kudaka penalti.

Kama sio mbili au tatu. Ndicho ambacho alifanya juzi. Aliwanyanyua mashabiki jukwaani akiwaambia atacheza penalti.

Ni kweli anaweza kuwa anataka kudaka lakini kama umri ungekuwa umemtupa mkono asingeweza kufanya chochote. Kwa nini mpaka sasa anafanya chochote? Kwa sababu Juma ana hamu ya kucheza soka.

Ana hamu ya kuendelea kukaa langoni. Matokeo yake anabakia kuwa mchezaji anayetajwa kufanya mazoezi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini.

Sio kwa makipa tu hadi kwa wachezaji wa ndani.

Kabla ya kujituma sana mazoezini, Juma anapenda kucheza sana. ana hamu na mchezo wenyewe. Hiki ndicho kinachoshangaza. Wachezaji wengi uuchoka mchezo wenyewe.

Uchoka kusafiri kwa Mabasi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Mwili unagoma. Lakini Juma ana kiu kila siku ndio maana bado yumo.

Baada ya kuondoka katika timu kubwa za Kariakoo alienda Mbeya kucheza Mbeya City, akaenda Kagera kucheza Kagera Sugara, amerudi anacheza KMC. Kote anakopita anakasirika akiwekwa benchi. Sio kwamba anataka apangwe kwa sababu ya jina lake, hapana, kwa sababu ya mazoezi yake na anajiona yuko fiti.

Pamoja na yote haya, Juma bado sio yule yule. Hawezi kuwa vile vile miaka 19 baadae.

Tatizo kubwa kuna vijana wamekuja baadae na wamechezea nafasi. Nafasi ya Tanzania One ilikuwa wazi baada ya Juma kuondoka lakini vijana wameichezea.

Vijana wetu hawajui thamani ya kuwepo katika timu kubwa wala kuwepo katika kikosi cha Taifa Stars. Wanafanya mazoezi ya kawaida na wanacheza soka la kawaida tu. wanaishi kwa mazoea.

Hawaimariki zaidi na maisha yamekuwa rahisi zaidi kwao kwa sababu wanapata pesa nyingi. Wakishasaini mkataba mpya baada ya miaka miwili wananunua gari zuri na kupost Instagram. Basi.

Ni changamoto kwao kuona Juma amerudi katika lango la Taifa Stars na hapana shaka atarudi tena na tena katika mechi za kufuzu kombe la dunia hatua ya makundi kombe la dunia, kisha mechi za kufuzu Afcon kuelekea Cameroon 2021.

Mambo mawili zaidi wanaweza kujifunza kupitia kwa Kaseja ninayemuona miaka 19 baada ya mechi ile ya Zamalek ni kwamba Juma ametulia sana langoni. Anajua kujipanga yeye mwenyewe na kuwapanga walinzi wake.

Pili, Juma amebadilika. Anaweza hata kucheza katika timu ya Pep Guardiola kutokana na uwezo wake wa kucheza mpira kwa miguu akianzisha pasi kutoka nyuma. Hana wasiwasi na staili hii ya kisasa.

Anapiga pasi kuanzia nyuma na akirudishiwa mpira kwa miguu hana papara.

Lakini pia nimemtazama Juma wa juzi, bado amebakia kuwa yule yule anayeweza kupiga pasi ndefu kwa mtu wa mbele na mpira ukamfikia alipo.

Kifupi ni kwamba anaweza kufanya ‘counter attack’ kwa kupiga pasi ndefu ya vipimo ambayo inaweza kuzalisha bao kwa timu yake wakati sekunde chache zilizopita shambulizi lilikuwa katika lango lake.

Shukrani pia ziende kwa kocha wake, Etienne Ndayiragije aliyekuwa kocha wake, KMC na sasa amemuamini katika kikosi cha timu ya taifa. Soka letu lina tatizo kubwa na umri na sio uwezo.

Hatuwapendi wachezaji ambao tumewahi kuwasikia sana. Hata kama bado wana uwezo tunataka kuwaondoa.

Kocha huyu Mrundi amekaa na Kaseja kwa msimu mmoja. Ameona ubora wake. amemtathimini kwa kumlinganisha na makipa wengine ambao anakutana nao katika Ligi. Huyu ni kocha mzoefu katika Ligi yetu. Amefundisha Mbao na KMC kabla ya kutua Azam. Anamjua Kaseja vema. Pengine ni tofauti na Emmanuel Amunike ambaye hajafundisha klabu yoyote nchini zaidi ya Taifa Stars.

Katika hali halisi uwezo ni kitu cha msingi kuliko umri. Mashabiki na viongozi wa Tanzania wanapenda wachezaji wapya.

Naambiwa Kaseja alikuwa amekasirika kwa kutochaguliwa katika timu iliyokwenda Misri kwa sababu aliamini kuwa takwimu zake ni bora kuliko makipa wanne waliochaguliwa na Emmanuel Amunike kwenda Misri.

Hata hivyo hakuna ambaye angeweza kusikiliza kilio chake kwa sababu tu kila mmoja aliamini kwamba Juma Kaseja amezeeka.

Juzi ameonyesha kwanini alistaili kwenda Misri. Na kwa jinsi makipa wetu wa sasa ambavyo hawaeleweki, hauwezi kujua Kaseja atakaa langoni mpaka lini.