HISIA ZANGU: Hatima ya Samatta Aston Villa ikishuka hii hapa

MTU mmoja aliniuliza kuhusu swali hili majuzi. Nini hatima ya Mbwana Samatta kama klabu yake Aston Villa itashuka daraja mwishoni mwa msimu? Villa hawapo mahala salama na kuna dalili nyingi kwamba huenda wakashuka daraja mwishoni mwa msimu.

Mechi zao zilizobaki ni ngumu wakati huu wakishika nafasi ya pili kutoka mkiani. Wana pointi 25 ingawa walio juu yako wana tofauti ya pointi mbili tu. Bournemouth, Watford, West Ham wana pointi 27. Lakini Brighton wanaoshika nafasi ya 15 wana pointi 29 tu.

Kimahesabu Villa wanaweza kubakia Ligi Kuu. Tatizo ni mechi zao za mkononi. Inabidi wapambane hasa. Inabidi wacheze na West ham, Arsenal, Everton, Liverpool, Man United, Wolves, Crystal Palace na Chelsea.

Hii sio kazi ndogo. Hapo kwa Arsenal, Liverpool, Manchester United na Chelsea pana kazi nzito katika dakika hizi za lala salama. Mashabiki wengi wanatamani kujua hatima ya kijana yao kama Aston Villa itadidimia shimoni na kushuka daraja.

Ni ngumu kujua hatima ya Samatta. Ni kwamba atakuwa amemaliza miezi sita tu ya mkataba wake wa miaka minne. Hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa ni rahisi kwa Samatta kuondoka Aston Villa kama wakishuka daraja.

Mawakala wa Samatta ni wazungu. Lazima waliangalia mahala ambapo Villa ipo na wakaweka baadhi ya vipengele katika mkataba wake. uzoefu wangu katika soka la Ulaya unaniambia kwamba mazungumzo baina ya mchezaji na klabu huwa yanazingatia mambo mengi.

Kwa timu ambayo ina mwelekeo wa kushuka daraja kuna wachezaji ambao wanaingiza vipengele vya kutocheza Ligi daraja la kwanza endapo klabu itashuka. Hawa huwa wanawekewa dau fulani (Release clause) kwa timu ambayo itamtaka mchezaji husika.

Kwa mfano, Villa wanaweza kuweka release clause kuwa Samatta anaweza kuuzwa dau la pauni 20 milioni kama Villa ikishuka daraja. Lakini pia mkataba wa Samatta nao una mengi. Hiki kinaweza kuwa sio kipengele pekee kuhusu suala la kushuka au kutoshuka daraja.

Kuna suala la bonasi pia. Inawezekana kuna kipengele ambacho kinasema Samatta atapata kiasi fulani cha pesa kama timu isiposhuka daraja. Kama lingekuwa suala la ubingwa nina uhakika kuwa Samatta pia angewekewa kipengele cha kupata kiasi cha pesa kama Villa ikitwaa ubingwa. Hata hivyo kiasi hicho cha pesa kisingeweza kuwa kikubwa kulinganisha na wenzake ambao safari wameianza zamani.

Kila siku nasisitiza umuhimu wa vipengele tofauti katika mkataba wa mchezaji. Lakini kila siku nasisitiza kwamba mkataba ni baina ya pande zote mbili. Upande wa mchezaji na upande wa klabu. Baada ya hapo vipengele vinaunganishwa kwa maslahi ya kila upande.

Huku kwetu mchezaji analetewa mkataba na klabu. Sidhani kama kuna wachezaji wanaoweka masharti yao katika mkataba. Mara nyingi wanaangalia burungutu la pesa na kusaini. Vipengele vingi vinawabana hao.

Turudi katika suala la Samatta. Uzoefu unaonyesha kwamba hata Villa wenyewe watatamani kumuuza Samatta na mastaa wengine kama wakishuka daraja. Mastaa kama akina Jack Grealish, Mahamoud Trezeguet, Tyrone Mings wapo hatarini kuuzwa endapo Villa watashuka.

Hawa ni mastaa wenye mishahara mikubwa na klabu huwa zinauza mastaa wake kwa sababu ya kupunguza gharama za kuendesha klabu. Klabu inaposhuka upoteza pesa nyingi ikiwemo zile za mauzo ya haki za televisheni. Klabu haipati tena pesa nyingi kwa kucheza daraja la kwanza. Haki za mauzo ya televisheni kwa Ligi daraja la kwanza zipo chini.

Lakini hata wadhamini mbalimbali wa Villa, hasa wale wadhamini wanakuu wanaokaa kifuani katika jezi huwa wana vipengele vya mkataba vinavyopunguza malipo kwa klabu kama itashuka na kwenda daraja la chini.

Wachezaji wenye mishahara mikubwa kama akina Grealish na Samatta watauzwa. Hii ndio sababu klabu nyingi ambazo hazina uwezo mkubwa wa kipesa huwa zinapata wakati mgumu wa kurudi Ligi Kuu. Ni klabu chache ambazo zinashuka na kupanda papo hapo kama vile Newcastle United.

Turudi kwa Samatta mwenyewe. Nini hatima yake kama Villa ikishuka? Ataweza kubakia Ligi Kuu ya England? itategemea na atakavyoendelea kucheza vizuri hata kama Villa itashuka Ligi Kuu. Hatima yake anayo mwenyewe zaidi katika mechi hizi ngumu zilizobaki.

Uwezekano wa kubakia Ligi kuu ni mkubwa. Mpaka sasa amefanya vema katika maeneo tofauti. Kwanza kabisa ana bao moja katika Ligi Kuu na bao moja katika fainali za michuano ya kombe la Ligi. Sio rekodi mbaya.

Kuna klabu zitakuwa zimemfuatilia kumjua zaidi tangu alipotua England. kwa wale ambao watakuwa hawamjui au wamemsahau basi watakumbushwa kuhusu rekodi zake za Ubelgiji, na jinsi alivyowafunga Liverpool, kisha watajumlisha mwendelezo wake wa kile alichofanya akiwa na Villa yeye kama yeye.

Kwa hilo bado Samatta ana soko. Majuzi Newcastle walikuwa wanalaumiana kwa kutomchukua Samatta baada ya kufunga mabao mawili akiwa na Villa. kuna klabu nyingi za England zilimtaka kabla hajatua Villa zitarudi katika njia.

Ni wazi kwamba hatafunga mabao mengi lakini endapo Villa watashuka watamuangalia tu jinsi gani alivyotumia nafasi chache alizopata akiwa na Villa. Wataangalia udhaifu wa Villa na kisha kupima namna gani aliweza kutumia nafasi chache alizopata. Mpaka sasa Samatta hajapata nafasi nyingi zaidi ya kukimbikimbia tu uwanjani huku Villa wakiwa hawamchezeshi ipasavyo. Ndio maana watu wengi huwa wanalia na akina Grealish.

Lakini mwisho zaidi kumbuka kwamba Samatta yupo katika mikono salama ya mawakala wajanja zaidi kuliko yule wa zamani ambaye alishindwa kumpatia Samatta timu kubwa licha ya kuongoza kwa kufunga kule Ubelgiji msimu mmoja kabla ya huu. Hawa wanajua cha kufanya na wanajua namna ya kumuweka sokoni kuliko mimi. Na hasa soko hili hili la England ambalo Samatta anama-tani kuendelea kucheza.