HII IMEKAA VIPI KWA WACHEZAJI YANGA?

Thursday July 16 2020

 

By DK. SHITA SAMWELI

Siku zote Katika mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba ni kawaida sana kusikia vizisingizio mbalimbali pale inapotokea mmojawapo amefungwa.

Sababu za kufungwa hutafutwa kila kona na mara nyingi unaweza usisikie sababu hizo kwa viongozi bali utazikuta kwa washabiki kindaki ndaki wa vijiweni ambao huwa pamoja na watani zao.

Kuna sababu moja ambayo nimesikia na kuisoma katika mitandao ambao washabiki wanailalamikia ambayo imenifanya nitambae na makala ya hii.

Unaambiwa washabiki wa jangwani wanadai kuwa kocha aliwachezesha mastaa wawili ambao walikuwa hawakao fiti kutokana na kutokucheza kwa muda mrefu.

Kama vile haitoshi mwingine akadai kuwa kocha amechezesha wachezaji ambao walikuwa hawajapona vizuri hivyo uwanjani walikuwa mzigo tu kwa wengine.

Mwingine akajibu mapigo kwa kuwa kama ni majeruhi mbona Simba ina mchezaji wa aina hiyo ambayo ni Shomari Kapombe ambaye inasemekana alipata mejaraha katika mchezo wao na Azam FC.

Advertisement

Hii imekaa vipi kwa wachezaji wa Yanga? Kufungwa goli 4-1 na Simba siku ya jumapili katika mchezo wa nusu fainali FA kunaweza kulichangiwa na sababu hizo zilizotajwa na mashabiki wa vijiweni?

Mabishano hayo yamenipa hamasa kutoa ufahamu juu ya kucheza na majeraha yakiwa hayajapona vyema na pamoja na kutocheza muda mrefu na kuingia kucheza mechi yenye ushindani.

Kinachojiri mchezaji akicheza na mejeraha yasiyopona vizuri

Haishangazi katika mazingira yetu ya Kiafrika mwanasoka anapokuwa tegemewa aidha kuamua kudanganya kupona na kucheza au lah akalazimishwa kucheza akiwa ametumia dawa za maumivu.

Mchezaji naye ni binadamu kushawishika kudanganya ili tu apangwe kucheza kikosi cha kwanza jambo ambalo humpatia bonasi ikiwamo ile anayopewa endapo atafunga au kuibuka ushindi.

Kawaida mara nyingi kiashiria kikubwa cha mchezaji kuwa hajapona vyema ni kuhisi maumivu katika eneo la jeraha.

Kucheza mchezo ukiwa na maumivu ni jambo ambalo sio sahihi kiafya kwani kunaongeza ukubwa wa tatizo. Jeraha linapotoneswa mara kwa mara ni chanzo cha kujijeruhi upya na hivyo kuchelewa kupona.

Maumivu kwa mwanamichezo aliye majeruhi ni ishara kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Maumivu yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati na makali. Yanaweza kuwa ni majeraha ya mfupa, misuli, mishipa ya fahamu na tishu nyingine za mwilini.

Panapotokea jeraha mwili hujibu mapigo kwa kutuma askari mwili kwa ajili ya kukarabati neneo hilo. Mlipuko wa kinga ya mwili ndio chanzo cha mtu kuhisi maumivu, kufa ganzi, kuvimba, kupata joto na kubadilika rangi ya ngozi. Hali hii ndio kitabibu huitwa inflammation.

Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi hudhani kuwa maumivu yanapopungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza. Pasipo kufahamu kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Mara yingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo uwapo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.

Unapobainika na wataalam wa tiba za michezo kuwa una majeraha ya mfupa na nyuzi ngumu (tendon na ligaments) fahamu kuwa itachukua muda kupona kabisa na kurudi mchezoni.

Mwanamichezo anahitajika kujifahamu na kujidhibiti binafsi na maumivu yake ikiwamo kujua yanachokozwa na mambo gani, je yanaanzaje wakati wakuanza, katikati au mwishoni baada ya mazoezi/mchezo?

Vema pia kufahamu kuwa maumivu yanauma unapominywa au yanakuwepo tu yenyewe, je yanasambaa au yanaibukia sehemu nyingine. Kila tabia ya maumivu ya mwili hutoa picha ya chanzo chake na ukubwa wake.

Wataalam wa tiba za afya za michezo huweza kugundua na kutibu maumivu, kuyatathimini madhara yake kiujumla na huku wakitambua mjongeo wa mwili ambao unaweza kuchochea tatizo hilo kuendana na jeraha lilipo katika mwili.

Baadhi ya makocha, viongozi na mashabiki ndio wanakawaida ya kushinikiza wachezaji walio na majeruhi na maumivu kuwapa dawa za maumivu na kuwalazimisha kushiriki mchezo huku wakijua wazi wana majeraha na hawako imara.

Ikumbukwe kuchoma sindano na kunywa dawa za maumivu zinakwenda kuondoa maumivu na kukupa utulivu kwa muda tu na si kukarabati jeraha na kuliponesha kabisa.

Hata pale anapopona mfupa, msuli au tishu zilizojeruhiwa kwa mara nyingine, hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa kwani tishu hizo zinapungua uimara kuweza kuhimili michezo na mazoezi.

Ni vizuri kuepuka kumchezesha mchezaji au kucheza akiwa na maumivu au majeruhi.

Ikimbukwe kuwa uwepo wa maumivu unachangia viungo vya mwili kutofanya kazi vizuri. Hivyo anapocheza uwanjani huonekana kabia hawakao timamu.

Mchezaji ambaye hajacheza muda mrefu

Ni kweli kama mchezaji hajachezeshwa siku nyingi anaweza kuwa mzigo uwanjani hii ni kutokana na ukweli kukaa muda mrefu nje kunachangia wepesi wa mchezaji kupungu

Kwa kawaida mwili wa binanadamu unapokaa muda mrefu bila ya kufanya kazi misuli huweza upata tatizo la kuwa na mkazo hivyo kuwafanya wakose wepesi hivyo kucheza chini ya kiwango.

Vile vile wachezaji wasipocheza muda na kwa kipindi walichokuwa wamejitenga wanaweza kupata tatizo la uzito mkubwa kutokana na ulaji holela wa vyakula.

Hali kama hizi ni kweli kabisa mambo haya yanaweza kumfanya mchezaji kukosa umakini.

Hivyo wale mashabiki waliolalama kuhusu kufungwa kwao na kuituhumu timu yao na kocha wao wanaweza kuwa na hoja ya msingi .

Advertisement