HATARI: Kupiga pasi za mabao ndio zao England

Saturday December 8 2018

 

By LONDON, ENGLAND

LIGI Kuu England inarudi tena wikiendi hii na macho ya wengi yatakuwa huko Stamford Bridge wakati Chelsea itakapowakabirisha Manchester City.
Itakuwa mechi ngumu itakayotegemea ufundi wa wachezaji matata kwenye timu hizo Eden Hazard kwa upande wa Chelsea na Kevin De Bruyne kwa upande wa Man City. Wabelgiji hao wataonyeshana ubabe. Kwenye mechi hizo, kutaonekana wakali wa kulipa pasi za mwisho zile zinazoleta mabao ili kuamua mechi. Hii hapa ndio orodha ya mastaa watano wanaoongoza kwa kupiga pasi za mabao kwa mechi zilizochezwa kwenye Ligi Kuu England hadi sasa.

5.Christian Eriksen- asisti 6
Tottenham Hotspur walikumbana na ubatizo wa moto dhidi ya mahasimu wao wa London Kashazini, Arsenal walipokutana nao kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita. Kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochetino kilikumbana na kipigo cha mabao 4-2 mbele ya Arsenal na kuwasahaulisha kabisa ushindi wao waliopata kwa vigogo Chelsea na Inter Milan kwenye mechi zilizotangulia. Ubora wa kikosi cha Spurs unahitaji umahiri wa wachezaji wengi akiwamo kiungo Christian Eriksen, ambaye amehusika  kwenye asisti nyingi kuliko mchezaji yeyote katika kikosi hicho kwa mechi za Ligi Kuu. Eriksen amepiga asisti sita.

4.Eden Hazard- asisti 6
Supastaa wa Chelsea, Eden Hazard alianza msimu vizuri sana kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa miezi miwili ya karibuni mabao na asisti zimekauka, amekuwa hana maajabu. Lakini, hilo si shida, kwani tayari ameshafunga mabao saba na kuasisti mara sita kwenye ligi hiyo na kuifanya Chelsea kuwa kwenye orodha ya timu nne za juu kwnye msimamo wa Ligi Kuu England. Kocha Maurizio Sarri atamhitaji Hazard arudi kwenye ubora wake hasa kwa mechi ya wikiendi hii dhidi ya wababe Manchester City. Chelsea inashika namba nne kwa sasa na pointi zao 31.

3.Raheem Sterling- asisti 6
Winga wa Manchester City, Raheem Sterling anafurahia soka la ubora wake chini ya kocha Pep Guardiola. Fowadi huyo Mwingereza anafunga na kutoa pasi za mabao kwenye kikosi hicho kwa msimu huu, akiwa amehusika kwenye asisti sita. Man City wapo kwenye kiwango matata kabisa na kupewa nafasi ya kuubeba ubingwa wa ligi msimu huu wakiwa hawajapoteza  mechi yoyote kwenye ligi hiyo. Wikiendi hii watakumbana na kigogo wakati watakapokipiga na Chelsea ya kocha Maurizio Sarri.

2.Aaron Ramsey- asisti 6
Arsenal wamekuwa vizuri msimu huu chini ya kocha wao Unai Emery. Wanacheza kwa kiwango bora kabisa wakiwa hawajapoteza mechi yoyote kwenye ligi tangu walipochapwa mara mbili mwanzoni mwa msimu dhidi ya Manchester City na Chelsea. Kwenye kikosi chao kuna mastaa wengi wapo vizuri, lakini hatari zaidi ni Aaron Ramsey, ambaye amehusika kwenye asisti nyingi kwenye kikosi hicho. Ramsey ndiye mchezaji aliyeasisti mara nyingi kuliko yeyote kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akiasisti mara sita.

1.Ryan Fraser- asisti 7
Bournemouth wamekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu. Ukiwatazama kwenye msimamo wapo nafasi ya saba wamewazidi hadi Manchester United wakiwa na pointi 23 baada ya kuwachapa Huddersfield 2-1 nyumbani. Jambo hilo halionekani kuwa ni sapraizi kwani Eddie Howe ameonyesha kuwa yeye ni kocha bora. Staa Ryan Fraser amekuwa mtu muhimu kweli kweli kwenye kikosi hicho kwa sasa, akihusika kwa asisti  saba na kuwa kinara wa kupiga pasi za mwisho za  mabao kwenye Ligi Kuu England msimu huu.


Advertisement