Gwambina wana jambo lao FA

Friday February 21 2020

By Saddam Sadick,Mwanza

WAKATI  Yanga ikiwa jijini Tanga kujiwinda na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union utakaopigwa keshokutwa Jumapili, wapinzani wake kwenye mechi ya Kombe la FA, Gwambina FC tayari wametua jijini Dar es Salaam kuweka mipango sawa ya kuwamaliza vigogo hao.

Yanga itakuwa kibaruani uwanja wa Mkwakwani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare mechi tatu mfululizo hivyo inahitaji ushindi ili kurejesha furaha kwa mashabiki wake.

Baada ya mchezo huo, Yanga itakuwa nyumbani kuwakaribisha vinara hao wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kundi B, katika mchezo wa Kombe la FA utakaopigwa Februari 26 ukiwa ni hatua ya 16 Bora kusaka tiketi ya kutinga Robo Fainali.

Katibu Mkuu wa Gwambina FC, Daniel Kirai alisema malengo ya kwenda Dar es Salaam mapema ni kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kusonga hatua inayofuata.

Alisema wanahitaji kutumia mchezo huo kujitangaza zaidi, huku akifafanua kuwa uongozi umejipanga kutoa sapoti katika mashindano yote hasa akili kubwa ikiwa kwenye FDL kuhakikisha wanapanda daraja msimu ujao.

“Tumeamua kuwahi ili kuweka mambo sawa na kuzoea hali ya hewa, kumbuka huu ni mchezo muhimu sana kwetu kujitangaza, pia uamuzi huu ni kwa kushauriana na benchi la ufundi ambapo tunapaswa kuheshimu maelekezo yao," alisema Kirai.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Novatus Fulgence alisema kikosi chake kipo fiti na wanaendelea kujiweka sawa kuhakikisha wanaweka historia kwenye michuano hiyo.

“Tuna malengo makubwa sana katika mashindano haya, hatudharau mchezo wowote kwa sababu hii ni timu ya ushindani na tumejipanga kuacha historia kwa msimu huu,” alisema Fulgence.

Advertisement