Gwambina FC kuivuruga au kuibeba Yanga

Muktasari:

Yanga ndiyo timu pekee katika Ligi Kuu msimu huu ambayo haijapoteza mchezo wowote.

Yanga inashuka uwanjani leo kuivaa Gwambina katika mchezo wa kusaka kujiamini zaidi kwa mchezo ujao dhidi ya watani zao, Simba.

Usindi wa Yanga leo utaifanya timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa raha zaidi licha ya sare pia inaweza kuwapa uongozi hadi matokeo ya Azam FC dhidi ya Dodoma Jiji.

Wapinzani wa Yanga katika mchezo wa leo, Gwambina, hawana mwenendo mzuri wa ligi, baada ya kushindwa kupata ushindi kwenye michezo mitatu iliyopita.

Ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union na kuchapwa mabao 3-0 na KMC katika mchezo uliofanyika Oktoba 30.

Wageni hao wa Ligi Kuu, Gwambina watatakiwa kuwa makini na nyota wa kigeni wa Yanga, ambao wameonyesha kuwa mwiba mkali katika kufumania nyavu, kwani ni kipa pekee, Farouk Shikalo, ambaye hajafunga.

Licha ya kutokuwa na mfungaji mwenye mabao mengi, Yanga imeonyesha kuwa na uhitaji wa nguvu wa ushindi katika kila mchezo kwa kutafuta nafasi ya bao kwa mfugaji yeyote.

Umuhimu wa ushindi katika mchezo wa kesho kwa Yanga ni kujiandaa na mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Simba, ambao msimu huu unaweza kuwa ndiyo mchezo wao mgumu zaidi unaofikiriwa.

Baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mtibwa, Kagera Sugar, Biashara United na KMC, Yanga imeongeza kujiamini katika kila mchezo wanaoshuka uwanjani msimu huu, huku Jumamosi wakiwa na jaribio gumu zaidi katika mbio za ubingwa.

Mabingwa watetezi, Simba, ambao wamepoteza michezo miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting, waliibuka na kuisambaratisha Mwadui FC, isiyo na mwenendo mzuri kwa mabao 5-0.

Na sasa watakuwa wakiiangalia Yanga hii leo kama itapoteza ili kuisimamisha Jumamosi na kupunguza pengo la pointi walilonalo la pointi sita na mchezo mmoja mkononi.

Gwambina inayonolewa na kocha Fulgence Novatus itakuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji wake kinda, Meshack Abraham mwenye mabao manne, ambayo ni sawa na yale ya Meddie Kagere(Simba), Obrey Chirwa(Azam), Yusuph Mhilu (Kagera Sugar) na Adam Adam wa JKT Tanzania, wote wakiongozwa na Prince Dube wa Azam mwenye mabao sita.

Kurejea kwa Paul Nonga kumempa faraja kocha Novatus, ambaye anaamini kuwa kama atakuwa katika kiwango bora akishirikiana na wenzake wanaweza kuipa Gwambina matokeo bora.

“Tunaiheshimu Yanga, ni timu kubwa na ina wachezaji wengi wa kigeni, lakini hilo halitufanyi kuiogopa kwani itakuwa kwetu kesho (leo), itakuwa mechi yao ya kwanza kupoteza mchezo,” alitamba Novatus.

Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze alisema malengo yao ni kuondoka na pointi tisa Kanda ya Ziwa, baada ya kuzifunga KMC na Biashara United.

“Hatuwezi kuidharau Gwambina, ni timu nzuri licha ya mechi iliyopita kupoteza. Tunachotaka ni ushindi ili tupande kileleni kwenye msimamo wa ligi, nahitaji wachezaji wangu kuendelea kujituma,” alisema Kaze.

Mchambuzi Ally Mayay alisema ushindi wa Yanga leo unaweza kuwa manufaa zaidi kama Azam itapoteza dhidi ya Dodoma Jiji, ili kuikabili Simba wakiwa kileleni.

“Ujue unaposhinda mechi unajenga kujiamini na hasa unapoelekea katika mechi kubwa ya watani wa jadi. Kwa sababu mara nyingi mwenendo wa mechi za nyuma unasaidia kujenga saikolojia ya wachezaji au kuipunguza. Ndiyo maana Yanga na Simba zitahitaji kupambana kushinda mechi zao kabla ya kukutana zenyewe Jumamosi,” alisema.