Gwambina: Hatuogopi, Nonga yupo

KOCHA wa Gwambina FC, Flugence Novatus anasema; “Najua mchezo utakuwa mgumu lakini tuko nyumbani hivyo, tutapambana kupata pointi tatu na hilo linawezekana mbona.

“Najua tunakutana na timu kubwa yenye wachezaji wazuri na haijapoteza mchezo hivyo, leo ndio itakuwa mara yao ya kwanza kupoteza kwenye uwanja wetu wa nyumbani.

“Hatuogopi ukubwa wa timu yao kwani yoyote anaweza kupata ushindi licha ya kwamba, wakati mwingine matokeo ya soka yanakuja na bahati lakini hawatatoka salama kwani, hatutakubali kupoteza tena mchezo wa pili mfululizo,” alisema Novatus.

Novatus alisema anachofurahi ni kuona mshambuliaji wake mzoefu, Paul Nonga akirejea katika kikosi hicho na atakuwa mmoja ya wachezaji watakaoikabili Yanga leo.

“Nonga alikuwa majeruhi ndio maana walikuwa haonekani kwenye kikosi muda mrefu kwani, aliumia mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Biashara United, alikaa nje mechi mbili nikamtumia mechi na Simba (Septemba 26) nikiamini amepona kabisa, lakini akajitonesha tena kwenye mchezo huo hivyo akakosa mechi tano ziliofuata lakini atakuwepo kesho (leo) dhidi ya Yanga kwa sababu amepona kabisa.

“Nimefurahi kuona amerejea kwani, ataongeza nguvu katika kikosi changu kwa sababu ni mchezaji mzoefu hivyo uwepo wake lazima utakuwa na manufaa kwetu. Kuna mtu ataumia kwa sababu ya uwepo,” alisema Novatus.