Guardiola asema sizitaki mbichi hizi

Muktasari:

  • Kocha wa City, Pep Guardiola ameikana rekodi hiyo na kudai haikuwa lengo lake, badala yake anafurahishwa zaidi na kuwania ubingwa katika ligi kuliko rekodi hiyo ya kibabe ya Arsenal iliyowekwa katika utawala wa kocha aliyepita, Arsene Wenger,“Kila mtu ananiuliza kuhusu jambo hilo, nilisema haiwezi kutokea.

LONDON, ENGLAND.UTARATIBU ni uleule wa ‘sizitaki mbichi hizi.’ Ndicho alichosema Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola baada ya kuambuliwa kichapo kutoka kwa Chelsea juzi Jumamosi katika pambano la Ligi Kuu England kikiwa kichapo chao cha kwanza msimu huu.

City ililala mabao 2-0 kutoka kwa Chelsea, mabao yaliyofungwa na kiungo, N’Golo Kante katika kipindi cha kwanza na bao la beki wa kimataifa wa Brazil, David Luiz katika kipindi cha pili na hivyo kukomesha mwendo wake mdundo katika ligi hiyo.

Kipigo kinaiacha Liverpool ikiwa ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi msimu huu baada ya mechi 16 na City kwa mara nyingi imeshindwa kuifikia rekodi ya Arsenal ambayo msimu wa 2003/04 ilicheza msimu mzima bila ya kupoteza pambano.

Kocha wa City, Pep Guardiola ameikana rekodi hiyo na kudai haikuwa lengo lake, badala yake anafurahishwa zaidi na kuwania ubingwa katika ligi kuliko rekodi hiyo ya kibabe ya Arsenal iliyowekwa katika utawala wa kocha aliyepita, Arsene Wenger,

“Kila mtu ananiuliza kuhusu jambo hilo, nilisema haiwezi kutokea. Hatupo hapa kwa ajili ya kuwa timu iliyoshindikana au timu ambayo haijafungwa msimu mzima. Tunataka kuwa mabingwa. Haijalishi. Tunakuwa na pointi nyingi kuliko wapinzani wetu. Kwa sasa Liverpool wako vizuri kuliko sisi,” alisema Guardiola.

“Tupo katika Mwezi Desemba. Kama ukiniuliza Liverpool inaweza kutwaa Ligi Kuu nitasema ndio. Kama ukiniuliza Tottenham, Arsenal au Chelsea zinaweza kutwaa ubingwa nitasema ndio. Hakuna mchezo wowote duniani ambapo timu moja au mchezaji mmoja atashinda kila kitu. Ni jinsi ambavyo unapoteza mechi na jinsi ambavyo tunataka kucheza. Mpinzani anapokuwa bora inabidi useme hongera,” alisema Pep.

Hata hivyo, licha ya kutosema ukweli, lakini msimu uliopita Guardiola aliweka lengo na nia ya kuwa timu ya kwanza katika Ligi Kuu England kufikisha pointi 100 baada ya kuonekana kufurahia kuliko kiasi katika pambano dhidi ya Southampton ambapo walishinda mechi na kufikisha pointi 100. Kwa matokeo ya juzi, Guardiola sasa anakuwa amepoteza mechi tatu za ligi kwa jumla dhidi ya Chelsea na hii inakuwa mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine zote za Ligi Kuu alizocheza nazo tangu awasili misimu miwili iliyopita.

Katika pambano la juzi makocha wote walichezesha vikosi vyao katika staili iliyofanana, hakuna kocha aliyeanza na mshambuliaji asilia wa kati. Wakati City ilianza na Raheem Sterling kama mshambuliaji wa kati huku ikimuacha nje, Gabriel Jesus aliyeingia katika kipindi cha pili, Chelsea ilianza na Eden Hazard kama mshambuliaji wa kati.

Guardiola ambaye licha ya kikosi chake kupoteza pambano hilo lakini kilitawala mechi, alitania yeye na kocha mwenzake, Maurizio Sarri walikuwa wamepanga kucheza katika mfumo wa soka unaofanana.

Mapema kabla ya pambano hilo, wapinzani wao Liverpool walikuwa ugenini dhidi ya Bournemouth na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu huku staa wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah akionyesha makali yake kwa kufunga hat trick.

Kwa pointi hizo tatu huku City ikichapwa ugenini, Liverpool sasa imekaa kileleni ikiwa na pointi 42 dhidi ya City yenye pointi 41 na mpaka baada ya raundi ya 16 Liverpool haijapoteza pambano lolote.

Wikiendi ijayo Liverpool itakuwa na mchezo mgumu Anfield itakapocheza na mahasimu wao Manchester United.

Manchester City itakuwa ikijaribu kufuta aibu itakapocheza dhidi ya Everton.