Guardiola aivulia kofia Liverpool

Muktasari:

Pep Guardiola amesema Liverpool ilikuwa timu tishio katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na amesifu ubora wa kikosi hicho.

London, England.Kocha wa Manchester City Pep Guardiola, amesifu kiwango bora cha Liverpool katika mashindano ya Ligi Kuu England msimu huu.

Guardiola alisema Liverpool ilikuwa timu yenye ushindani mkali tangu mwanzo wa msimu huu na amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kupambana.

Kocha huyo alisema anashukuru Liverpool iliwasukuma kuongeza kasi yua kutwaa ubingwa wa England kwa mara ya pili mfululizo.

“Tunawapongeza Liverpool, tunawashukuru sana, wametusaidia kuongeza kasi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich na Barcelona.

Guardiola alisema kuwa ni jambo la kujivunia kutwaa ubingwa ukiwa na pointi 98 nyuma ya mpinzani ambaye alitoa upinzani wa kuwania ubingwa hadi dakika ya mwisho.

“Ni fahari kufikisha pointi 98, tumepambana. Tuliongeza ubora wetu msimu huu na Liverpool ilikuwa chachu kwetu kuongeza kiwango cha uchezaji,”aliongeza Guardiola.

Licha ya kukosa ubingwa, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema anajivunia kiwango bora cha wachezaji wake walichokionyesha msimu huu.

Alisema kitendo cha kumaliza katika nafasi ya pili kwa pointi 97 ni fahari kwake kwa kuwa ni pointi za juu kwa mshindi wa pili.

“Tulitaka kuandika historia na tumeandika. Timu imepiga hatua kubwa kulinganisha na msimu uliopita. Vijana wameipeleka timu katika kiwango kingine, nimependa,” alisema kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund. Wakati Man City ikiichapa Brighton mabao 4-1, Liverpool ilishinda 2-0 ilipovaana na Wolves.