Griezmann awaza Man U na Man City

Muktasari:

Mfaransa huyo anadaiwa kuwa na mpango wa kwenda ama Manchester United au Manchester City, akiamini huko atapata nafasi ya kurudi kwenye kiwango bora.

Barcelona, Hispania. Mshambuliaji wa Barcelona, Antoine Griezmann anatafuta namna ya kutimka kwenda kutafuta mahali ambapo atapata nafasi ya kucheza na kujiamini ili kurudisha makali yake.

Mfaransa huyo anadaiwa kuwa na mpango wa kwenda ama Manchester United au Manchester City, akiamini huko atapata nafasi ya kurudi kwenye kiwango bora.

Mshambuliaji huyo alitua Barcelona akitokea Atletico Madrid kwa ada ya Pauni 108 milioni katika dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana lakini amekuwa akihusishwa na mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Nou Camp baada ya kushindwa kucheza soka la kiwango kilichotarajiwa.

Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, klabu mbili za Manchester mara kadhaa zimekuwa zikifuatilia uwezekano wa kunasa huduma ya Griezmann na kwamba anaweza kushawishika kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Griezmann amefunga mabao 14 na kuasisti mara nne katika mechi 45 za michuano yote aliyocheza msimu huu, lakini ameanzishwa mechi moja tu kati ya nne za mwisho alizotumikia wababe hao.

Alicheza dakika mbili tu katika sare ya 2-2 dhidi ya klabu yake ya zamani ya Atletico, Jumanne iliyopita. Wakati Griezmann akinyanyuliwa kwenye benchi ili aingie, kaka yake, aliandika ujumbe kwenye Twitter: “Nataka kulia, siriazi.”