Greenwood atengwa kwa muda

Manchester, England. Mason Greenwood ametakiwa kufanya mazoezi mwenyewe bila kujichanganya na wachezaji wenzake wa Manchester United kwa siku kadhaa.

Mshambuliaji huyo, ambaye sasa ana miaka 18, alirudi Carrington Alhamisi kwa mara ya kwanza baada ya safari yake ya kuichezea England kugeuka shubiri.

Lakini sasa ametakiwa kuja uwanja wa mazoezini baada ya kocha Ole Gunnar Solskjaer na kikosi kizima kumaliza mazoezi.

Greenwood na Phil Foden walitimuliwa katika kikosi cha timu ya taifa kutokana na kuvunja kanuni za kujikinga na corona nchini Iceland kwa kualika wasichana katika hoteli iliyofikia timu ya England.

Man United ilisisitiza kuwa Greenwood atalazimika kupimwa kipimo cha corona kabla ya kujiunga na wenzake.

Hatakuwepo katika mchezo wa leo wa kirafiki dhidi ya Aston Villa.

Solskjaer anapanga kukutana na kijana huyo kuzungumzia shutuma zake, ingawa hatapewa adhabu yoyote.

Anaweza kutumika wakati Man United ikicheza mchezo wake wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace wa Septemba 19.

Wakati huo huo, Judd Trump alisema ilikuwa hadithi mbaya kusikia tukio la beki wa kati wa Man United, Harry Maguire.

Mchezaji huyo namba moja wa mchezo wa Snooker alikuwa na beki huyo siku ya tukio akisherehekea ‘birthday’ ya miaka 31.