Goti la Sane litapasuliwa hivi

Muktasari:

Sane (23) aliamua kutotaka kufanyiwa upasuaji na daktari bingwa Dk. Ramon Cugan ambaye ndiye anayependelewa zaidi na Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.

KATIKA kuonyesha dili lake la kutua Bayern Munich bado lipo kwenye damu yake, winga wa Manchester City, Leroy Sane atafanyiwa upasuaji na daktari bingwa wa klabu hiyo.

Nguli huyu wa upasuaji wa mifupa Dk. Christian Fink wa Australia ndiye pia anaitumikia Timu ya Taifa ya Ujerumani ndiye amekuwa chagua la winga huyo anayehusishwa na uhamisho wa kutua kwa miamba hiyo ya Ujerumani.

Sane wiki tatu zilizopita alipata majeraha ya nyuzi ngumu ya ligamenti ya mbele ya goti la kulia wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Liverpool. Upasuaji huo wa kisasa wa saa nzima wa ligamenti ijulikanayo kitabibu kama Anterior Cruciate Ligament-ACL inayoshikilia mifupa ya ungio la goti la kulia unatarajiwa kufanyika leo Ijumaa kule Australia.

Sane (23) aliamua kutotaka kufanyiwa upasuaji na daktari bingwa Dk. Ramon Cugan ambaye ndiye anayependelewa zaidi na Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.

Dk. Cugan kutoka katika Jiji la Barcelona ndiye aliyewafanyia upasuaji wachezaji kadhaa wa Manchester City waliowahi kupata majeraha mabaya ya goti ikiwamo Benjanmin Mendy, Kevin De Bruyne na Ilkay Gundon.

Beki wa kushoto, Mendy alipata majeraha mabaya ya goti yaliyomweka nje msimu uliopita alitibiwa na nguli huyo na tayari amepona na ameshaanza mazoezi na klabu yake.

Pamoja na matibabu hayo mazuri ya Dk. Cugan kwa wachezaji wa Man City haikuweza kumfanya Sane (23) kubadili maamuzi yake. Wachambuzi wa soka wanahusisha uamuzi huo wa Sane ni kama wa kujipendekeza kwa Bayern ili kuendelea kuweka hai dili lake la kutua katika klabu hiyo. Ingawa kwa jicho la kitabibu uamuzi kama huu ni sahihi kabisa kwani haki za mgonjwa zinaweka wazi kuchagua daktari anayetaka kumtibu.

Wachambuzi wa soka wa Ujerumani wanasema uamuzi huo ni sawa, kwani Sane ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ujerumani ni vizuri atibiwe na daktari anayejulikana vyema na Wajerumani.

Pamoja na tukio hilo, Klabu ya Man City imekuwa tulivu na kuheshimu uamuzi wa winga huyo wa kuchagua matibabu kutoka kwa Dk.Fink.

Mara baada ya upasuaji huu Sane anatarajiwa kuwa nje katika ya miezi 7-9 hivyo ni dhahiri atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu ili kuweza kupona kabisa.

Kocha wake, Guardiola alisema Sane anaweza kurudi kati ya Februari au Machi, akaeleza zaidi kuwa bado ni mchezaji wao na hajawahi kusema kama anataka kuondoka na kutua Bayern Munich.

Ingawa kwa kawaida upasuaji wa goti unaweza kuwa wa kizamani wa kupasua goti kwa njia ya jeraha la mkato na aina ya pili ni upasuaji wa kisasa wa matundu madogo.

Leo nitawapa ufahamu juu ya upasuaji wa kisasa wa matundu unaojulikana kitabibu kama Arthroscopic Surgery ambao ndiyo utakautumiwa na Dk.Fink kwa Sane.

Usiyoyajua kuhusua upasuaji huo Sane alipata jeraha hili baada ya goti lake kwenda uelekeo hasi ambao si rafiki wa mjongeo wa nyuzi ya ACL, hivyo kuifanya kupata shinikizo kubwa la ghafla na kuvutika kupita kiwango chake na kukatika.

Upasuaji huu huenda ukawa ni wa kisasa wa matundu wa goti ambao unahusisha matundu na kutumbukiza kifaa maalumu chenye taa, kisu na kikapu.

Daktari hupasua matundu na kupenyeza kifaa hicho ndani ya tundu lililo mkabala na la pili ambalo hupitisha hewa yenye msukumo ili kupanua tishu, hivyo kuongeza wigo.

Aina hii ya upasuaji huwa na faida kubwa ya kupunguza uvujaji wa damu nyingi kwani hakuna jeraha kubwa, bali ni vitundu. Mgonjwa hutoka mapema kwani baada ya saa 24 huruhusiwa na pia kovu huwa ni zuri lisiloharibu umbo asili la mwili. Nyuzi ya ACL iko eneo la mbele ya goti ambayo huwa na kazi ya kuliimarisha ungio la goti kwa kuzuia mifupa ya goti isiende mjongeo hasi.

Baada ya Sane kufanyiwa uchunguzi wa kina wa tishu kwa kutumia picha za MRI ilionyesha nyuzi ya ACL ya goti la kulia imekatika na kuanishwa kama daraja la tatu la jeraha la ligamenti.

Aina hii ya jeraha la ligamenti huitaji upasuaji ili kuikarabati nyuzi hiyo au kuichimbia pale mahala ilipokwanyuka au kuiunga pale ilipokatika pande mbili.

Katika kuikarabati nyuzi ngumu iliyojeruhiwa upasuaji huu upo wa aina mbili ikiwamo wa kwanza inayohusisha kupandikiza tishu ambayo huchukuliwa kutoka katika nyuzi ya tendoni ya mgonjwa au kwa mtu mwingine aliyejitolea.

Nyuzi ngumu ya ligamenti ya ACL inaweza kuondolewa yote kwa njia ya upasuani na kupandikiziwa tendoni nyingine ambayo hukua na kuwa imara kama ya hapo awali.

Tendoni ni nyuzi ngumu inayounganisha msuli kwenye mfupa hufanana sawa kiutendaji kimaumbile na ligamenti ambazo huunganisha mfupa na mfupa. Kabla ya upasuaji huu unaochukua saa nzima, mgonjwa hupewa dawa ya usingizi na kulala usingizi mzito kiasi cha kutohisi maumivu na wala kutokuwa na ufahamu wowote wa upasuaji huo.

Daktari kwa kutumia ujuzi wa upasuaji huchukua tendoni sehemu nyingine ikiwamo katika goti, misuli ya nyuma ya paja au ile ya nyonga na hatimaye kuipandikiza na kuwa mbadala wa ligamenti liyoharibika.

Daktari hutoboa tundu katika mfupa wa juu ya goti (paja) na chini ya goti (ugoko) na kuipachika tendoni hiyo na kuibana na boriti. Baada ya miezi kadhaa tishu hiyo ya tendoni hukua na hatimaye huwa ndiyo ligamenti mbadala.

Baada ya upasuaji mgonjwa hutakiwa kuwa mtulivu kwa kutoufanyisha shughuli yoyote na huvishwa kifaa tiba maalumu mfano wa P.O.P ili kuutuliza na kuulinda mguu wenye jeraha.

Maelekezo kadhaa atapewa ikiwamo kufanya ‘dressing’ ya jeraha hilo na kulala huku mguu ukinyanyuliwa juu kuzidi kifua kwa kuulaza mguu juu ya mito kadhaa. Baadaye mgonjwa huwa katika uangalizi wa kliniki ya ufuatiliaji wa maendeleo yake na hapo baadaye akigundulika yupo katika hatua za juu za uponaji huanzishiwa mazoezi tiba yaani physical therapy.

Kiungo wa Liverpool Ox-lade Chamberlain alipata majeraha kama haya na kuukosa msimu uliopita, hivyvo ndivyo inavyotarajiwa pia kwa Sane ambaye anatarajiwa kuwa nje kwa muda mrefu.