Gor Mahia yatoa onyo kwa Simba, Yanga, Mbao FC

Muktasari:

  • Bandari FC (Kenya), ambao walimaliza katika nafasi ya pili, kwenye ligi kuu ya Kenya (KPL), msimu uliopita na Mbao FC (Tanzania), ndio timu mbili zilizojumuishwa kwenye kipute hiki kwa mara kwanza, zikichukua nafasi ya Kakamega Homeboyz na JKU ya Zanzibar.

Nairobi, Kenya- Mabingwa mara mbili wa kombe la SportPesa, klabu ya Gor Mahia ya Kenya imetoa angalizo kwa timu zingine zitakazoshiriki makala ya tatu ya michuano hiyo, ambayo itakayofanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia Januari 22-27 mwakani.

Gor Mahia, ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe hilo, linaloandaliwa na kampuni ya kubeti ya SportPesa na kushirikisha timu nane, nne kutoka Kenya na nyingine nne kutoka Tanzania, wamewataka wapinzani kujiandaa kisaikolojia kwani haitakuwa kazi rahisi kuwavua ubingwa.

“Tunafahamu kuwa haitakuwa rahisi kutetea ubingwa kwa mara ya tatu, lakini tumejipanga na tungependa kuwaambia wapinzani wetu wajiandae kwa mapambano, lazima tulibakishe kombe kwenye makabati yetu”, Alisema Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier.

Makala ya tatu ya kombe la SportPesa yatashirikisha timu nane, ambao ni mabingwa watetezi Gor Mahia, Kariobangi Sharks, Bandari FC na AFC Leopards, zote kutoka Kenya huku kutoka Tanzania, kukiwa na timu nne ambazo ni mabingwa watetezi wa VPL, Simba SC, Yanga FC, Mbao FC na Singida FC.

Bandari FC (Kenya), ambao walimaliza katika nafasi ya pili, kwenye ligi kuu ya Kenya (KPL), msimu uliopita na Mbao FC (Tanzania), ndio timu mbili zilizojumuishwa kwenye kipute hiki kwa mara kwanza, zikichukua nafasi ya Kakamega Homeboyz na JKU ya Zanzibar.

Makala ya kwanza ya kipute hiki, yalifanyika mwezi Juni, mwaka jana, katika uwanja wa taifa, Jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, ambapo Gor ilishinda na kupata nafasi ya kucheza na Everton FC, wakafungwa 2-1.

Makala ya pili, yakafanyika ugani Afraha Nakuru, nchini Kenya, ambapo mabingwa hao walipata nafasi ya kwenda Goodison Park, nchini Uingereza kukipiga na Everton FC, baada ya kuhifadhi taji lao, kwa kuifunga Simba SC, 2-0. Mchezo wa Goodison Park, uliopigwa Novemba 6, mwaka huu, uliishuhudia Kogalo wakitandikwa 4-0.