Gor Mahia yamchorea giza Oliech

Muktasari:

  • Akiwa na miaka 34, alitia saini mkataba wa mwaka na nusu na Gor ambao unapaswa kumlipa Sh350, 000 kila mwezi

Nairobi. Ukistaajabia ya Musa, basi hujaona ya Gor Mahia. Mwishoni mwa wiki iliyopita straika mzoefu wa Gor Mahia, Dennis Oliech alisusia mchuano wa CAF Confederation katika Kundi D dhidi ya Walgeria Hussein Dey.

Fowadi huyo alijiengua kikosini  kisa mshahara wake. Ripoti zinaarifu Oliech aliamua kujitoa kikosini baada ya kwenda benki na kupata kwenye akaunti yake kawekewa  mshahara mdogo kinyume na ule alioafikiana na klabu alipokuwa akisaini mkataba. Kwa masala mtaaani, huku ni kuchorewa giza.

“Sidhani kama atajiunga na timu tena mpaka pale matakwa alizoahidiwa na klabu kipindi akisaini mkataba nao zitakapotimizwa,” alifichua mtu mmoja wa karibu wake ambaye aliomba jina lake libanwe.

Oliech alijiunga na Gor Januari mwaka huu ikiwa ni miaka miwili baada yake kutangaza kustaafu soka. Akiwa na miaka 34, alitia saini mkataba wa mwaka na nusu na Gor ambao unapaswa kumlipa Sh350, 000 kila mwezi. Mshahara huu ni kando na kiasi kingine cha Sh3.5 milioni aliyolipwa kama fedha za usajili.

Hata hivyo, juzikati Oliech inasemekana hakuamini macho yake alipokwenda benki na kukuta amewekewa Sh100,000 tu kwenye akaunti yake.

Kwa hasira, Oliech aliamua kususia timu ikiwemo kukosa kuhudhuria mazoezi ya mwisho  ya Jumamosi kabla ya timu kuvaana na Hussein Dey.

Aidha taarifa nyingine zimedai Oliech aliamua kuilenga timu baada ya klabu kukosa kumlipa salio ya Sh2 millioni ya fedha za usajli.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor, Lordvic Omondi Aduda alipuzilia mbali tetesi hizo klabu inajaribu kumchorea giza Oliech kwenye malipo yake.

“Ndio anatudai lakini kuna makubaliano ya utaratibu wa jinsi tutakavyomlipa deni lake. Hii haihusiani kabisa na yeye kutohusishwa kwenye mechi ya Hussein Dey. Halafu hiyo Sh100,000 ilikuwa ni timizo la ahadi ya mwenyekiti wa klabu (Ambrose Rachier) aliyoitoa kwa timu kama wangetinga hatua ya makundi ya CAF Confederation,” Aduda alidai huku akisisitiza  kukosekana kwa Oliech ilikuwa uamuzi wa kiufundi tu na wala sio eti kagoma.

Tangu Oliech ajiunge na Gor, tayari amepachika mabao manne kutokana na mechi saba alizocheza licha ya nyingi ya michuano hiyo kuanza benchi.