Gor Mahia yaleta mbogi ya mtu tano

Muktasari:

Gor bado haijakamilisha usajili wa Djabel anayetajwa kuwa mridhi wake Francis Kahata licha ya klabu yake ya Rwanda Rayon Sports kuthibitisha kufikia makubaliano na Kogalo.

Nairobi. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia wamethibitisha kukamlisha usajili wa wachezaji watano huku ule wa kiungo fundi Mrwanda Djabel Imanishimwe ukiwa bado.

Klabu hiyo imethibitisha kuzinasa sahihi ya kiungo Tobias Otieno na beki wa kulia Abdalla Ashura kutoka Sony Sugar na vile vile beki wa kati Elvis Ronack kutoka Nzoia Sugar ambao kila mmoja katia sahihi mkataba wa miaka minne.

Na kuzidisha nguvu zaidi kwenye safu yake ya mashambulizi baada ya kuwapoteza wachana nyavu Jacques Tuyisenge na Meddie Kagere, Gor imewasajili winga Curtis Wekesa kutoka Nairobi Stima inayoshiriki divisheni ya pili pamoja na straika Dennis Oalo aliyeipachika Stima magoli 24 msimu uliopita. Wachezaji hao vile vile wamesaini mkataba wa miaka minne.

Hata hivyo Gor bado haijakamilisha usajili wa Djabel anayetajwa kuwa mridhi wake Francis Kahata licha ya klabu yake ya Rwanda Rayon Sports kuthibitisha kufikia makubaliano na Kogalo.

Kulingana na maelezo yaliyonazwa na safu hii ni kwamba Gor imeshakubaliana na mchezaji huyo kuhusiana na suala la mshahara wake pamoja na fedha za usajili. Hata hivyo mazungumzo baina ya klabu hizo mbili ndio bado.

Gor imeripotiwa kuafikiana na Djabel kuwa itamlipa mshahara wa Sh150, 000 kila mwezi huku ikimlipa vile vile Sh1 milioni kama fedha za usajili.

Aidha itatakiwa kuilipa klabu ya Rayon Sh3 milioni kama fedha za uhamisho wake Djabel aliyeipachikia magoli 29 na kutoa asisti 53 katika kipindi cha miaka mitano waliyoichezea.