Gor Mahia yajifua tayari kuwavaa Everton

Monday November 5 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia leo imefanya mazoezi yake ya mwisho nchini England kujianda na mchezo maalum wa kirafiki, dhidi ya Everton FC utakaopigwa kesho kuanzia saa 7:00 usiku kwa saa za Uingereza, sawa na saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ugani Goodison Park.

KOgalo mabingwa wa kombe la SportPesa, walifanyia mazoezi hayo katika uwanja wa mazoezi ya USM Finch Firm inayomilikiwa na wenyeji wao Everton FC, ambapo baadaye leo watatembelea uwanja wa Goodison Park, kwa ajili ya ukaguzi kabla kipute cha kesho.

Wakionesha kuwa na ari na morali kubwa, nyota wa Gor Mahia, wakiongozwa na Kocha wao, Muingereza Dylan Kerr na kocha msaidizi, Zedekiah ‘Zico’ Otieno, walifika uwanjani hapo na kupasha mwili, licha ya kuwepo kwa baridi kali, kabla ya kuelekea hotelini kwao.

Hali ya hewa ya Jiji la Liverpool, kwa leo ilikuwa mbaya sana, kiasi cha kufikia chini ya nyuzi joto sita (-6), tofauti na ilivyokuwa walipowasili katika taifa hilo linalongozwa na Malkia, lakini halikuwazuia kutinga mazoezini.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mazoezi, Kocha Kerr alisema licha ya hali ya hewa kuwalemea, wako tayari kukabiliana na Everton FC huku akithibitisha kuwa hakuna majeruhi mpaka sasa katika kikosi chake.

“Mazoezi ya leo yalikuwa mazuri sana, kila mchezaji anaonyesha kuwa na morali na itoshe kusema tu kuwa tuko tayari kwa ajili ya mechi ya kesho. Hatujapata tatizo lolote, vijana wako fiti, hakuna majeruhi, tuko sawa’” alisema Kerr.

Mabingwa hao mara 17 wa KPL, walipata fursa ya kukutana na Everton kwa mara ya pili, baada ya kuifunga Simba FC ya Tanzania 2-0, mapema mwaka huu, katika mechi ya fainali ya kombe la SportPesa, iliyopigwa ugani Afraha Nakuru.

Mara ya kwanza kukutana na Everton FC, Ilikuwa mwaka jana katika uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam, ambapo Everton FC, ambao walifanya safari yao ya kwanza kuja Afrika, walishinda 2-1, mabao yakifungwa na Wayne Rooney na Kieran Dowell. Bao la Kogalo lilifungwa na Jacques Tuyisenge.

Viingilio na Tiketi.

Habari njema ni kwamba, viingilio kwa ajili ya mechi hiyo vimepunguzwa hadi dola moja (Ksh132) kwa watoto na Dola 5 (Ksh660) kwa watu wazima.

Advertisement