Gor Mahia imeifunza kitu Bandari kwa Shandy

Muktasari:

Timu ya Bandari ililazimishwa sare tasa na Shandy katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi

Mombasa. BANDARI FC sasa inaelekeza juhudi zake zote kuhakikisha inapata ushindi ama matokeo yatakayoifanya ifuzu kwa raundi nyingine ya mashindano ya Caf Confederation Cup inapokutana na Al Ahly Shandy ya Sudan hapo Ijumaa.

Naibu kocha wa timu hiyo ya mkoani Pwani, Ibrahim Shikanda aliambia Mwanaspoti jana kuwa wanakutana na Shandy wakati wanarekebisha makosa waliyofanya wakati walipokutana na Gor Mahia katika mchezo wa KPL Super Cup juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

“Wapinzani wetu Gor mahia walipata nafasi moja pekee ‘on target’ na wakaitumia kufunga bao la pekee na la ushindi kwa timu hiyo hali sisi tulipata nafasi nyingi lakini tukazipoteza. Kocha Bernard Mwalala anafanyia kazi idara hiyo ya ushambulizi,” akasema Shikanda.

Mkufunzi huyo alisema kwamba wameendelea na maandalizi yao huko jijini Nairobi ambako ndiko wataondokea kuelekea huko Sudan kwa pambano lao la marudio la kupigania timu itakayosonga mbele kwenye mashindano hayo.

“Tunaamini japo tulitoka sare tasa hapa nyumbani, tuna matumaini makubwa ya kuibuka washindi. Tunakwenda kupigania kushinda mechi ama kutoka sare ya kufungana ili tuweze kufuzu kwa raundi nyingine,” akasema Shikanda.

Alisema jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa hakuna mchezaji yoyote ambaye alijeruhiwa wakati nwa mechi yao na Gor na hivyo, kikosi kitakachokwenda Sudan kitakuwa na wachezaji wenye afya njema.

“Mchezaji yoyote atakayepangwa kwenye mechi yoyote atacheza vizuri na atatumika kiwanjani kuhakikisha timu inapata ushindi. Wachezaji wetu wako na moyo mkubwa wa kupata ushindi dhidi ya Shandy ili kuwafurahisha mashabiki wao na Wakenya kwa ujumla,” akasema.

Timu ya Bandari ililazimishwa sare tasa na Shandy katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi, matokeo ambayo hapo awali Mwalala alisema hayakuwa mabaya na kuwa wana matumaini ya kushinda huko ugenini.