Gor Mahia ‘Kogalo’ itaivia mbele kwa mbele

Muktasari:

Tangu aliposhika usukani, Polack amesimamia sare tasa dhidi ya Aigle Noir kwenye dimba la CAF Champions League ilipochuana nayo ugenini Bujumbura, Burundi.

KOCHA mpya wa Gor Mahia, Mwingereza, Steven Polack amekiri licha ya kupata ushindi dhidi ya Bandari FC kwenye fainali ya Super Cup, kikosi chake bado hakijaiva kabisa.

Polack amekuwa nchini kwa wiki sasa tangu alipochukua nafasi yake Kocha Hassan Oktay aliyejiuzulu.

Tangu aliposhika usukani, Polack amesimamia sare tasa dhidi ya Aigle Noir kwenye dimba la CAF Champions League ilipochuana nayo ugenini Bujumbura, Burundi.

Mechi ya Bandari juzi Jumapili ilikuwa yake ya pili na hakika alishuhudia kikosi chake kikihangaishwa kwa kipindi kirefu kabla ya kuangukia bao la kipekee katika kipindi cha pili.

Mpaka sasa Gor imefanya usajili wa wachezaji 18 wapya baada ya kuwapoteza saba waliounda kikosi cha kwanza msimu uliopita.

Akitoa utathmini wake baada ya kutwaa taji lake la kwanza, Polack alisema kikosi chake bado hakijawa tayari ila anaamini kitaiva kadiri masiku yatakavyosonga.

“Kikweli hatukucheza mechi ya kuvutia ila wajua mwisho wa siku la msingi ni matokeo na wala sio ulivyocheza.  pamoja na hayo ni kwamba bado hatujaiva kabisa na kama unavyojua nina siku chache tu tangu nimefika huku, hivyo ndio naendelea kujaribu kuwaelewa wachezaji wangu. Bado nawajaribu na naamini nitaibuka na kikosi kizuri siku za mbeleni,” Polack alisema.

Ni kauli iliyoungwa mkono na nahodha mpya wa Gor, Kenneth Muguna akishikilia kuwa wanahitaji muda zaidi kuivisha.

“Tumesaini wachezaji wengi halafu hatukuwa tumecheza pamoja kwa muda mrefu kama wenzetu Bandari na ndio sababu kidogo walituhangaisha lakini tena si wajua Gor ni timu kubwa. Huu ushindi tuliuhitaji ili kutupa motisha ya kuanza msimu vyema,”