Gor Mahia, FKF kujadili suala la Super Cup

Wednesday November 14 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya (KPL), klabu ya Gor Mahia, wanatarajiwa kukutana na Shirikisho la soka nchini (FKF), kujadili tarehe ya mchezo wa Super Cup, dhidi ya mabingwa wa SportPesa Shield Cup, Kariobangi Sharks FC, ambao umepangwa kupigwa Desemba 2, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Gor, Ludovick Aduda, kupitia mtandao wa klabu hiyo, Gor Mahia itakaa meza moja na FKF, katika siku chache zijazo, kujadili ratiba ya mechi hiyo, itakayotumika kama mchezo wa kufungua pazia la msimu mpya wa KPL (2018/19), kwani unaingiliana na ratiba za mechi za mtoano za ligi ya mabingwa Afrika.

"Tumepanga  kukutana na FKF kujadili kwa kina kuhusu ratiba hii. Desemba 2, tumepangiwa kucheza na Kariobangi Sharks, wakati kila mtu anafahamu tutakuwa safarini kwenda Blantyre kucheza mechi ya CAF dhidi ya Nyasa Big Bullets. Inabidi tuliangalie upya swala hili, Aduda aliuambia mtandao wa Gor Mahia.

Mchezo huo, umepangwa kufanyika siku mbili kabla ya mtanange wa marudiano, wa ligi ya mabingwa dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi. Novemba 27, Kogalo watawaalika Nyasa Big Bullets ugani Kasarani, kabla ya kuwafuata kwao Blantyre Malawi, kwa ajili ya mechi ya marudiano utakaopigwa Desemba 4, mwaka huu.

Advertisement