Giniki awakimbiza Wakenya mbio za Haydom marathoni

Saturday November 10 2018

 

By Joseph Lyimo

Mbulu. Mwanariadha wa kimataifa Emmanuel Giniki ameshinda mashindano ya riadha ya Haydom marathon kilomita 21 Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, yaliyowashirikisha wanariadha zaidi 300 wa Tanzania, Kenya na Norway.

Giniki alifanikiwa kuongoza mbio hizo kwa saa 1:05:33 zilizofanyika kwenye viwanja vya Haydom wilayani Mbulu.

Mashindano hayo yamewashirikisha wanariadha wa Tanzania, Kenya na Norway yenye na lengo la kununua mashine ya mionzi ya CT scanner ya hospitali ya rufaa ya Haydom.

Mwanajeshi wa JWTZ Joseph Panga alikuwa wa pili kwa saa 1:05:37 na Mkenya Abraham Too akiwa wa tatu kwa saa 1:06:06

Mkenya Noah Kemei alishika nafasi ya nne saa 1:06:35 na mwanariadha Anthony Moya wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara alishika nafasi ya tano.

Kwa upande wa wanawake Mkenya Naomi Jepngetich alishinda mbio za marathoni kilomita 21, saa 1:14:14, Failuna Matanga wa jijini Arusha, alishika nafasi ya pili kwa saa 1:15:23 na Nathalia Elisante wa jijini Arusha alishika nafasi ya tatu saa 1:22:05.

Mashine hiyo ya CT scanner ina gharama ya Sh800 milioni, lakini kupitia mbio hizo zimepatikana sh100 milioni.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga akizungumza wakati akizindua mbio hizo leo Novemba 10 ameipongeza hospitali ya rufaa ya Haydom kwa ubunifu wa mbio hizo.

Mofuga ambaye ameshiriki mbio za kilometa mbili na kuibuka mshindi wa kwanza amesema kupitia mbio hizo wamekutanishwa watu wa Tanzania, Kenya na Norway.

Amesema kupitia mbio hizo watu wengi wamefanikisha kutunza afya zao hasa kwa magonjwa ambayo siyo ya kuambukizwa.

"Tumepunguza gharama kubwa za kutibu watu kwa kupitia michezo hivyo nawapongeza sana hospitali ya Haydom kwa kubuni mbio hizo za uchangishaji wa ununuzi wa mashine hiyo ya mionzi.

Mkurugenzi wa hospitali ya Haydom Dk Emmanuel Nuwass amesema lengo la mashindano hayo ni kufanikisha ununuzi wa mashine ya mionzi ya CT Scanner ya gharama ya sh800 milioni kwenye hospitali ya rufaa ya Haydom.

Dk Nuwass amesema kwenye mashindano hayo wamefanikiwa kupata sh100 milioni za ununuzi wa mashine hiyo.

Meneja wa benki ya CRDB Mkoani Manyara, Ronald Paul amesema kwa upande wao wameshiriki kwa kutoa sh10 bilioni za ununuzi wa mashine hiyo ya CT Scanner katika mbio hizo.

Mwanariadha wa zamani wa kimataifa John Stephen Akhwary amewapongeza wanariadha wote walioshiriki kwenye mbio hizo.

Akhwary amesema kupitia mashindano hayo anatarajia kupatikana kwa warithi wake katika mbio za riadha.

Katibu wa shirikisho la riadha Tanzania, Wilhelm Gidabuday amesema mashindano hayo ya Haydom marathon ni ya kipekee kwa mwaka huu katika kuchangia ununuzi wa mashine hiyo ya mionzi.

Gidabuday amesema mkoa wa Manyara una historia ya kipekee katika riadha nchini ndiyo sababu akashiriki kwenye mbio hizo za Haydom huku mbio nyingine zikiendelea leo jijini Dodoma.

Advertisement