Giggs amtabiria makubwa Bale

CARDIFF, WALES. KOCHA wa timu ya Taifa ya Wales, Ryan Giggs anaamini winga wake Gareth Bale ataonyesha kiwango kikubwa katika michuano ya Euro 2020, baada ya kuondoka Real Madrid ambako alikuwa hapati nafasi ya kucheza.

Bale ambaye alipata mafanikio makubwa akiwa na miamba hiyo ya Hispania ikiwa pamoja na kushinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa kwenye uhusiano mbaya na kocha wa sasa wa timu hiyo, Zinedine Zidane ambaye hakuwa anahitaji kumtumia kwenye kikosi chake.

Licha ya kwamba hakuwa anapata nafasi ya kucheza Real Madrid lakini alikuwa ni mmoja ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa ya Wales na Giggs anaamini kitendo chake cha kuihama Real kitafanya kiwango chake kuimarika zaidi.

“Haijalishi mtu ana ubora kiasi gani, lakini huwa anaimarika zaidi anapopata nafasi ya kucheza. Kutocheza mechi nyingi mfululizo kunashusha kiwango cha mchezaji husika, naamini hapo Spurs atatumika zaidi ya huko alipokuwa awali,” alisema.

Bale ambaye ni majeruhi kwa sasa ameenguliwa kwenye kikosi cha Wales kitakachocheza dhidi ya England katika dimba la Wembley Alhamisi ijayo, pia atakosa michezo mingine miwili dhidi ya Ireland na Bulgaria ya Uefa Nations League. Giggs anaamini mchezaji huyo atarudi kwenye kiwango chake kwa kuwa anafundishwa na Jose Mourinho.

“Yupo kwenye klabu ambayo inafundishwa na kocha mzuri, na alisema ana furaha ya kurejea.”