Giggs ampa onyo Cavani

MANCHESTER, ENGLAND. RYAN GIGGS amempa onyo na kumwambia straika Edinson Cavani anapaswa kugangamala kwelikweli ili kutamba kwenye kikosi cha Manchester United.

Straika huyo wa Uruguay, Cavani akiwa na umri wa miaka 33, alitarajia kutua Man United kwa uhamisho wa bure jana Jumatatu kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, akiripotiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Pauni 200,000 kwa wiki.

Lakini, gwiji wa Man United, Giggs alisema Cavani, ambaye aliachwa na Paris Saint-Germain Juni, atahitaji kuwa na muda kidogo kabla ya kuanza kuendana na kasi ya kikosi hicho cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Giggs alisema: “Cavani hatakuwa na shida ya ukubwa wa klabu. Ni mchezaji wa kiwango cha dunia, nadhani uzoefu wake utamsaidia.

“Macho ya wetu yataelekezwa kwake na kama atakuja basi ni lazima atalazimika kufanya kweli kwa sababu presha itakuwa kwake. Nadhani Man United inahitaji mshambuliaji wa kati. Wanahitaji mtu wa hivyo kuwafungia mabao. Bila ya shaka atalifanya hilo.”

Wasiwasi wa Giggs unakuja sehemu moja tu kwamba wachezaji wengi wa kutoka Amerika Kusini wamekuwa na wakati mgumu wanapotua kwenye kikosi cha Man United baada ya Radamel Falcao, Angel di Maria na Alexis Sanchez kuboronga.

“Mechi yangu ya pili dhidi ya Uruguay, Cavani alifunga. Alinivutia sana, kiwango chake kilikuwa moto. Lakini, Man United kuna Waamerika Kusini wengi wamekuja na wameshindwa kutamba. Falcao, Di Maria, Sanchez hivyo, Cavani anapaswa kugangamala kuonyesha tofauti,” alisema Giggs.