Ghost, Zico wamtoa rangi Wanyama

Muktasari:

Makocha hao aidha walikashifu kiwango cha Wanyama cha uchezaji kwa kusema alikuwa chini ya kiwango hasa kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Senegal

Nairobi. WAKUFUNZI wa zamani wa Harambee Stars, Jacob Ghost Mulee na Zedekiah ‘Zico’ Otieno wamemtoa rangi nahodha wa timu hiyo ya taifa kwa kusema hastaili kuwa kapteni.

Kwa kauli moja makocha hao wanashikilia mtazamo kuwa Wanyama anayekipiga katika klabu ya Tottenham Hotspurs kule Uingereza hana sifa za uongozi kitu kilichodhihirika wazi kule Misri.

Kulingana na Mulee aliyeiongoza Stars kufuzu kwa dimba la AFCON 2004 miaka 15 iliyopita, kati ya blanda zilizoshuhudiwa katika kikosi hicho ni ukosefu wa uongozi.

“Ukiniuliza mimi Wanyama sio kiongozi. Hana sifa hizo kabisa na huwezi kushiriki michuano ya kiwango hicho kama huna kiongozi mzuri.

“Hulka yake niya mtu mtulivu, nay eye sio mzungumzaji hivyo huwezi kumtegemea kuiongoza timu vyema na hili lilionekana wazi wazi kwenye mechi zote tatu alizocheza.

“Alishindwa kuwashauri wachezaji ilivyotakiwa, kuwatia morali na mambo kama hayo yanayohitajika kwa kiongozi yeyote” Mulee aliwaza.

Zico aliyeifunza Stars 2010 hadi 2011 alimtoa rangi Wanyama vile vile kwa kusema ule unahodha alipewa kutokana na kuwa anakipiga soka lake Uingereza ila sio kwa sababu ana sifa na vigezo vya uongozi.

“Uteuzi wa Wanyama kama nahodha wa timu kwangu haukuwa uamuzi sahihi, naamini alipewa ukaptini kutokana na anakopiga soka lake la kulipwa.

“Nahodha anahitaji kuwa ni mchezaji mpambanaji, anayesikizwa na wachezaji wenzake pamoja na benchi la ukufunzi, asiyechoka kuwasukuma wenzake timuni. Hizi sifa sikuziaona na Wanyama kabisa” Zico alisema.

Makocha hao aidha walikashifu kiwango cha Wanyama cha uchezaji kwa kusema alikuwa chini ya kiwango hasa kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Senegal ambapo uwepo wake hakuonekana kabisa.