Gemu 5 za ubingwa kwa Liverpool na Man City

Muktasari:

Mashabiki wengi watajiuliza kama Liverpool itafuta nuksi za miaka ya nyuma ya kuambulia kukamata nafasi ya pili. Liverpool ya Kocha Jurgen Klopp ina kikosi cha hatari ambacho kinajumuisha wakali wenye nguvu na spidi bila kusahau nguvu ya mashabiki yao.

WIKI iliyopita nilitabiri Liverpool ingeangukia pua kwa Manchester City, lakini matokeo yakawa tofauti kwani badala yake Liverpool iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Ingawaje ushindi wao umeacha maswali kutokana na utata uliosababishwa na Mwamuzi Michael Oliver na zile video za kumsaidia (VAR).

Hata hivyo, pamoja na matokeo hayo bado Liverpool na Man City ndio timu zenye ubavu wa kupigania ubingwa.

Wiki hii tutapumzika kidogo masuala ya utabiri wa mechi za Ligi kuu England, ambayo imesimama kwa sababu ya mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo kipute cha ligi kitarudi Novemba 23, mwaka huu.

Tuangalie wiki hii mechi tano za Liverpool na Man City ili kujua nani ana mteremeko na yupi mwenye kibarua kigumu kwenye safari ya ubingwa.

Man City inalia kunyimwa penalti mbili ambazo inaamini ingepata basi matokeo yangekuwa tofauti kwenye mechi ya Liverpool.

Ushindi wa Liverpool angalau umeongeza matumaini ya kumaliza kiu yao ya miaka 30 ya kutotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

Kufuatia ushindi wao wa mabao 3-1, sasa Liverpool ipo pointi tisa kwa Manchester City kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Liverpool inajitahidi kudumisha makali yake ya msimu uliopita kwani umahiri wa Man City ndio ulioifanya kukosa ubingwa. Pamoja na kuwa Liverpool ilifanikiwa kupata pointi nyingi 97 lakini Man City ililitwaa taji baada ya kujikusanyia pointi 98.

Mashabiki wengi watajiuliza kama Liverpool itafuta nuksi za miaka ya nyuma ya kuambulia kukamata nafasi ya pili. Liverpool ya Kocha Jurgen Klopp ina kikosi cha hatari ambacho kinajumuisha wakali wenye nguvu na spidi bila kusahau nguvu ya mashabiki yao.

Kucheza na Liverpool Anfield hakufai kwani yowe linalopigwa na mashabiki pale imekuwa ngumu kwa timu ngeni kupona.|

Mbwana Samatta alisimulia majuzi wakati alipotia mguu pale na timu yake ya Genk ya Ubelgiji akisema amecheza katika viwanja vingi lakini pale ni balaa.

Wakati Liverpool ipo vizuri sana na hasa kwenye fowadi ikiwa na Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino hali ni tofauti kwa Man City, ambayo beki yake ina matobo kibao.

Ni wazi Kocha wa Man City, Pep Guardiola anajutia kitendo cha kutoziba pengo la sentahafu, Vincent Kompany. Kibaya Zaidi timu hiyo ilipata pigo kufuatia kuumia kwa beki wao tegemeo wa kati, Aymeric Laporte, jambo ambalo limeimaliza kabisa.

Kibaya zaidi kipa wake namba moja, Ederson naye ameingia katika listi ya majeruhi.

Guardiola amejikuta anakuna kichwa kwa kupanga beki ya kujishikiza tu, kwa mfano kwenye beki ya kushoto ana Angelino, ambaye beki wa wa Kihispania aliye na uzoefu mdogo wa kucheza mechi mbili za Ligi Kuu England.

Katika beki ya kati amekuwa akiwatumia Fernandinho, ambaye nafasi yake halisi ni kiungo na mwenzake John Stones, ambaye anajulikana kwa kufungisha mara kibao.

Angalau kwenye nafasi ya kulia, yupo Kyle Walker, ambaye ndio mzoefu katika kikosi hicho.

Wakati ligi ikiwa imebakiza miezi saba kumalizika, Manchester City sasa imejikuta katika nafasi ya nne ikiwa pointi tisa nyuma ya Liverpoool inayoongoza ligi.

Hali ni mbaya kuwa Guardiola zaidi kwani hana nafasi ya kupumua kwani anakabiliwa na mechi ngumu kutokana na ujio wa madogo wa Chelsea wanaonolewa na Lampard.

Pale itakapoingia mwezi Desemba, Manchester City wana kibarua cha kuikabili Leicester City baadae watavaana na |wapinzani wao wa jadi, Manchester derby na baadae watakuwa na tripu ya kuivaa Arsenal.

Kwa ratiba hiyo ya hatari ya Manchester City inaweza kutoa mwanya kwa Liverpool kujihakikishia ubingwa wa mapema.

Ukizingatia Liverpool wamekuwa na rekodi inayotisha katika kipindi hiki kwani wamedondosha pointi mbili tu tangu kuanza kwa ligi.

Kutokana na ubavu wa timu za Liverpool na Manchester City, sasa tuangalie mechi tano za kila timu halafu watandika mkeka kazi kwenu kupima upepo mapema wa nani anaweza kuwa bingwa wa England msimu huu lakini mechi ni wazi zitatupa picha nzuri.

Man City:

Man v Chelsea (Nov 23)

Newcastle v Man City (Nov 30)

Burnley v Man City (Des 3)

Man City v Man Utd (Des 7)

Arsenal v Man City (Des 15)

Liverpool:

C.Palace v Liverpool (Nov 23)

Liverpool v Brighton (Nov 30)

Everton v Liverpool (Des 4)

B’mouth v Liverpool (Des 7)

Liverpool v Watford (Des 14)