Geita Gold Mine yawalaza Arusha United bao 1-0

Muktasari:

Mchezo huo uliopigwa leo katika uwanja wa Sheik Amri abeid ulishuhudiwa wenyeji Arusha United wakishambulia lango la wenyeji wao Geita mfululizo bila mafanikio baada ya mlinda mlango wa Geita Khomeiny Abubakar kuokoa mashuti yote.

Arusha. Timu ya Geita Gold Mine imefanikiwa kumaliza vizuri mzunguko wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania bara mara baada ya kuwafunga wenyeji wao Arusha United bao 1-0.
Mchezo huo uliopigwa leo katika Uwanja wa Sheik Amri abeid ulishuhudiwa wenyeji Arusha United wakishambulia lango la wenyeji wao Geita mfululizo bila mafanikio baada ya mlinda mlango wa Geita Khomeiny Abubakar kuokoa mashuti yote.
Dakika 45 ya kipindi cha kwanza kilimalizika huku Arusha united wakienda mapumziko wakiwa na kumbukumbu ya kukosa mashuti zaidi ya 12 ikiwemo la moja kwa moja lililopigwa na Malimi Busungu dakika ya 43 baada ya kufanyiwa madhambi na Ernest Mwalupani eneo la hatari.
Kipindi cha pili kilipoanza,  kibao kiliwageukia wenyeji Arusha united ambao walionekana kushambuliwa hadi langoni, mashambulizi yaliyozaa bao dakika ya 64 kupitia kwa mshambuliaji wao Ibrahim Kungu baada ya kumchenga mlinda mlango wa Arusha Shaibu Ally.