Geay kukiwasha huko Houston nusu Marathon

Muktasari:

  • Mbio hizo za umbali wa kilomita 21, zinatarajiwa kufanyika katika mji wa Houston nchini Marekani, ambapo atakua Mtanzania pekee atakaewakilisha nchi katika mbio hizo.

ARUSHA.MWANARIADHA Gabriel Geay anatarajia kuanza mwaka kwa kushiriki mbio ya ‘Houston nusu marathon’ zitakazofanyika Jumapili ya January 20 mwaka huu huko Marekani.

Akizungumzia maandalizi yake, Geay alisema bado anaendelea na mazoezi ya mbio hizo katika Uwanja wa Ilboru kilivyoko nje kidogo ya Jiji la Arusha chini ya Kocha Thomas Tlanka kwa ajili ya kuhakikisha anafanya vyema.

“Nimefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya hizi mbio kutokana na kujua umuhimu wake kwani ndio zinazonifungulia mwaka hivyo kubweteka na mazoezi na kwenda kufanya vibaya huko kutaniharibia CV yangu (wasifu wangu) ya mwaka huu.”

Geay alisema amejipanga kuwa na historia nzuri ya mbio zote atakazoshiriki mwaka huu za ndani na nje ya nchi ambazo anaamini akifanya vema itamwongezea nafasi ya kupata mialiko mingi zaidi na kubadilisha maisha yake kiuchumi.

“Riadha ndio mchezo ambao nimechagua kuucheza hivyo lazima nifanye mazoezi ya aina yake, maana naamini pia ndio mchezo utakaonitoa kimaisha hivyo mwaka huu nimepanga kutoka kiuchumi kupitia riadha” alisema Geay.

Mbio hizo za umbali wa kilomita 21, zinatarajiwa kufanyika katika mji wa Houston nchini Marekani, ambapo atakua Mtanzania pekee atakaewakilisha nchi katika mbio hizo.