Gaucho: Corona inaturudisha nyuma

Muktasari:

Ameelezea uzoefu wake kwamba kama mwanamke akikaa nyumbani anakumbana na changamoto tofauti kwani wengine wameolewa hivyo watakosa muda wa kufanya mazoezi.

MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Mwanahamisi Omary 'Gaucho' amesema ugonjwa wa corona ni changamoto kwa soka la wanawake kulinda viwango vyao.
Amesema tofauti na wanaume ambao miili yao ipo fiti na kwamba wana uwezo wa kurejea kwa kishindo.
Ameelezea uzoefu wake kwamba kama mwanamke akikaa nyumbani anakumbana na changamoto tofauti kwani wengine wameolewa hivyo watakosa muda wa kufanya mazoezi.
"Mwanamke ni rahisi kuridhika tofauti na mwanaume, mfano wale ambao wameolewa muda unakuwa mdogo wa kukaa na familia, kufanya mazoezi inakuwa ngumu,"
"Sisemei Simba pekee bali ni soka la wanawake kwa ujumla ingawa kuna wale ambao wanajua kabisa wanatakiwa wafanye nini,"amesema.
Kwa upande wake amesema amezoea kufanya mazoezi na kwamba alichagua soka kuwa kazi ya kumpa kipato cha maisha.
"Sijawahi acha kufanya mazoezi labda niwe naumwa hivi hivi mwili wangu hauwezi hata kidogo,"amesema