Gari la Azam limewaka sasa

Muktasari:

Azam ni moja kati ya timu 9 pekee zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikifanya hivyo msimu wa 2013-2014.

AZAM FC iliyotoka kupoteza pointi nane katika mechi tatu zilizopita usiku wa jana Ijumaa ilifanya kweli baada ya kuibamiza Biashara United ya Mara kwa mabao 2-1 katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara uliopigwa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Mabao ya kipindi cha kwanza kutoka kwa Idd Seleman 'Naldo' na beki Nicholas Wadada yalitosha kuifanya Azam ifikishe alama 13 na kuchupa toka nafasi ya 15 hadi ya  na kutoka ya 11 baada ya kushuka uwanjani mara saba na kuiacha Biashara katika nafasi ya 17 na alama zao nane baada ya kucheza michezo 10.
Azam iliuanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza iliandika bao la kwanza baada ya krosi ya Donald Ngoma kumalizwa wavuni kiufundi na Naldo lililokuwa bao lake la pili msimu huu na kwenye dakika ya 21 Wadada akafanya mambo kwa kufunga bao lake la kwanza katika ligi msimu huu akimaliza pasi ya kisigino ya Obrey Chirwa.
Biashara iliyotoka kuchezea kichapo cha 2-1 ugenini dhidi ya KMC katikati ya wiki, ilicharuka na kufanikiwa kuwabana Azam kabla ya kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Innocent Edwin dakika ya 32, likiwa bao lake la tatu mpaka sasa katika Ligi Kuu inayosimama kwa muda.
Kipindi cha pili licha ya timu zote kufanya mabadiliko na kushambuliana kwa zamu, hakukuwa na mabadiliko yoyote kwani hadi filimbi inaliza kuashiria dakika 90 zimemalizika Azam ilikuwa wababe kwa mabao 2-1.