Gareth Bale ajipanga kurudi tena Tottenham

Thursday September 17 2020

 

London, England. Tottenham ipo karibu kumsajili winga wake wa zamani, Gareth Bale kwa ada ya uhamisho wa mkopo wa Pauni 20 milioni.

SunSport iliripoti jana kuwa Spurs imekubali kuweka kitita hicho mezani kwa ajili ya kumrudisha winga huyo wa kimataifa wa Wales kutoka Real Madrid kwa ajili ya msimu huu.

Kikosi cha kocha Jose Mourinho kipo karibu zaidi kumsajili Bale kucheza tena Ligi Kuu England, huku nyota huyo wa miaka 31 akitamani zaidi kujiunga tena na Tottenham kuliko Manchester United, ambayo pia inamtaka.

Wakala wa Bale, Jonathan Barnett alithibitisha hilo juzi usiku aliponukuliwa akisema: “Gareth bado anaipenda Spurs. Tunazungumza kwa sasa. Huko ndiko anakotaka kuwa.”

Spurs inamtazama Bale kama mchezaji wao halisi licha ya kuondoka kwenda kujiunga na Real 2013, wakati huo akivunja rekodi ya usajili kwa ada ya Pauni 86 milioni.

Bale alitoa kauli ya kuzigonganisha klabu za Ligi Kuu England wakati alipotaka kumaliza jinamizi la kukaa benchi katika klabu ya Madrid, kutokana na kuwekwa nje na kocha Zinedine Zidane.

Advertisement

Mchezaji huyo pia aliishutumu miamba hiyo ya Mji Mkuu wa Hispania kwa kukataa usajili wake wa fedha nyingi kujiunga na Ligi Kuu ya China saa 11 kabla ya usajili uliopita kufungwa.

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy yupo tayari kukamilisha uhamisho huo na mtandao wa SunSport ulithibitisha kuwa makubaliano yapo karibu kufikiwa kwa Bale kurudi England.

Advertisement