Galana Secondary bingwa wa Pwani inayotesa kila mwaka kwenye raga

Wednesday April 3 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

MARIKEBUNI. NI jambo la kawaida kwa shule fulani kuwika kwenye michezo fulani ambayo huyatawala kwa kipindi kirefu.

Kwa shule ya Galana Secondary iliyoko Kaunti ya Kilifi mkoani Pwani imekuwa ikiwika kwenye mchezo wa raga ya wachezaji 15 mwaka hadi mwaka.

Uzoefu wa mchezo huo wa raga umeifanya shule hiyo ya Galana kutawala na kuwa mabingwa wa Pwani wa mchezo wa raga aidha kwa wachezaji saba ama wachezaji 15 kuhakikisha tangu mwaka 2015.

Kwa upande wa wachezaji saba, Galana imeshinda taji la mkoani miaka ya 2017 na 2018 na kumaliza nafasi ya pili mwaka huu. Kwa mchezo wa raga ya wachezaji saba, Galana imeibuka washindi miaka 2015 na 2016.

Ushindi huo unathibitisha Galana inafaa kutambuliwa kuwa shule ya kuunda wachezaji wenye vipaji ambao wanaweza kufika mbali wakati wanapoendelea kusoma shuleni hapo na hata baada ya kumaliza masomo yao.

Mwalimu Mkuu, Thomas Safari aliliambia Mwanaspoti ilipotembelea hapo shuleni wanajivunia kila mwaka wamekuwa wakiunda wachezaji wenye vipaji ambao kabla ya kumaliza masomo yao, hutakiwa na shule nyingine za huko bara.

Akifafanua, Safari anasema mnamo mwaka 2016 Emmanuel Mnyaka alichukuliwa na shule ya Upper Hill akiwa kidato cha tatu na hivi sasa ni mchezaji wa akiba wa klabu ya Menengai Oilers inayoshiriki kwenye Kenya Cup.

Mchezaji mwingine ni Calvin Kahindi aliyechukuliwa na Upper Hill mwaka 2017 zakiwa kidatio cha pili hali Stephen Baraza Gona akasajiliwa na Upper Hill mwaka jana alipokuwa kidato cha tatu. “Naamini hata mwaka huu, baadhi ya wachezaji wetu huenda wakapendeza shule nyingine,” akasema.

Meneja wa timu hiyo, Jerim Odima amesema ana imani vijana wake kufanya vizuri mwaka huu kutokana na matayarisho ya mapema waliyofanya. Alisema walishindwa na Kwale High kutokana na kuwa na madharau lakini sasa watakaza kamba kufanya vyema michezo ya kitaifa.

“Tulikuwa tushinde na kuhifadhi taji letu lakini wachezaji wetu wakachukulia madharau na tukashindwa kwa 15-3 na Kwale High katika mechi ya fainali. Sasa tumelirekebisha hilo na ni kuhakikisha tunashinda mwanzo hadi mwisho hasa kwa kuwa tuko nyumbani,” akasema.

Timu ya shule ya Galana ambayo ndio mabingwa wa Mkoa wa Pwani kwa mchezo huo, imepania kuwakilisha vyema kwenye ngazi ya kitaifa ikiwa na nia kubwa ya kufuzu kwa Michezo ya Shule za Upili ya Afrika Mashariki huko Dar es Salaam, Tanzania hapo Agosti.

KIkosi cha Galana kina Reuben Kalu (Nahodha), Victor Wabwire, Rajab Khamis, Brian Kombe, Mwanengo Mbogo, Elvis Kenga, Thomas Thoya, Baya Kitsao, Hamisi Mohamed na Jonah Mapenzi.

Wengine ni Suleiman Hassan, Alfan Salim, Musa Changamwa, Maxwell Odera, Justus Mwango, Japhet Mathew, Baraka Chivatsi, Tobias Nyawa, Thomas Happy na Cosmas Madubi.

Nahodha Reuben Kalu amesema watajitahidi kuihakikisha wanashinda taji la kitaifa kwani wana hamu kubwa ya kwenda Dar kwa michezo ya kanda ya Afrika Mashariki. Tuna hamu kubwa ya kuhakikisha tunafuzu kwa mechi za kanda hii ya Afrika kwa mara ya kwanza,” akasema Kalu.

Nahodha huyo alisema kamwe hawana wasiwasi wowote wa kukutana na timu yoyote kwenye michezo ya kitaifa yatakayofanyika Mombasa kuanzia Aprili 9.

“Tunataka kudhihirisha kuwa Pwani pia tunaweza kuibuka mabingwa wa kitaifa kwa mchezo wa raga,” akasema Kalu.

Advertisement