GSM: Kaze kutambulishwa kambini

KIKOSI cha Yanga kimerudi kambini jana asubuhi na leo watatangaziwa rasmi na uongozi baada ya mazoezi ya asubuhi kwamba, Kocha mpya ni Cedric Kaze raia wa Burundi anayeishi Canada.

Yanga ilimpiga chini Zlatko Krmpotic baada ya kutoridhishwa na soka lake na aina yake ya uongozi pamoja na uendeshaji wa mambo.

Kwa sasa wanapambana kuhakikisha Kaze anakamilisha mambo yake kwa wakati na kutua nchini mapema wikiendi hii kujiandaa na mechi ya Novemba 7 baada ya kusogezwa mbele tarehe ya awali Oktoba 18.

Akiwa Canada, Kaze amekuwa akipenyezewa taarifa kuhusu ubora wa wapinzani wake kuanzia Simba na Azam ambao, wana vikosi bora msimu huu akifanya mawasiliano hayo na kocha wa makipa Vladimir Niyonkuru.

Niyonkuru ndio kocha wa Kaze aliyemtanguliza mapema wakati akitakiwa kwa mara ya kwanza kabla ya kubadili uamuzi wake kutokana na masuala ya kifamilia.

Bosi wa GSM, Mhandisi Hersi Said amelithibitishia Mwanaspoti kuwa wako katika hatua za mwisho kabisa kumleta Kaze nchini baada ya kukubaliana kila kitu.

“Tunamsubiri yeye tu aseme anataka kuja lini nchini, tumeshakamilisha kila kitu kuhusu Kaze, tutakapokuwa tayari kwa ujio wake mtajulishwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Hersi, Kaze atatambulishwa kwanza kwa makocha na kuanzia sasa atakuwa akifanya mawasiliano ya karibu na kocha msaidizi, Juma Mwambusi ambaye aameanza kazi ya kukaimu nafasi ya kocha mkuu kuanzia jana.

Mbali na Mwambusi na wasaidizi wengine pia wachezaji watapewa taarifa rasmi na fursa ya kuwasiliana kwa karibu na Kaze, ambaye anatajwa kuwa ni muumini wa soka la pasi nyingi.

Awali, Kaze aliwahi kuiambia Mwanaspoti kwamba anakuja Yanga kurejesha heshima na kuifanya timu icheze soka la kuvutia sambamba na ushindi kwakuwa, kuna wachezaji wenye vipaji na ubora mkubwa kumpa matokeo. Pia, alisema kuwa Yanga inahitaji maboresho madogo na amekuwa akiifuatilia mara kwa mara.