GEORGE MASATU : Mambo haya yalimvuruga ataka kujiua-2

Muktasari:

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya ya beki wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Simba na Taifa Stars, George Magere Masatu alisimulia masahibu yaliyomkuta hadi sasa kuwa dereva wa gari la mizigo wakati alishacheza hadi soka la kulipwa kwa miaka saba huko Indonesia akilipwa mkwanja mrefu. Tuungane tena leo.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya ya beki wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Simba na Taifa Stars, George Magere Masatu alisimulia masahibu yaliyomkuta hadi sasa kuwa dereva wa gari la mizigo wakati alishacheza hadi soka la kulipwa kwa miaka saba huko Indonesia akilipwa mkwanja mrefu. Tuungane tena leo.

MZOZO WA NYUMBA

Masatu anasema mali zake na mkewe zilileta mgongano mkubwa hasa nyumba kwani ilijengwa kwenye kiwanja ambacho walipewa zawadi na mama mkwe pia nyumba iliandikwa jina la mke wake.

“Sijapata mali yoyote, kiukweli ilileta shida sana suala hili hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi, ingawa nyumba tulijenga kwenye kiwanja tulichopewa kama zawadi na mama yake.

“Hicho kiwanja, kwanza mama mkwe alitaka kutapeliwa sasa aliponieleza mimi wakati huo nacheza Simba nilienda moja kwa moja kwa bosi mmoja wa Wizara ya Ardhi, wakaenda kukagua eneo na kubaini kwamba kweli anataka kudhulumiwa, hivyo walikiokoa kiwanja hicho.

“Mama mkwe alifurahi sana nimemsaidia hivyo aliona atupe kama zawadi, lakini ndiyo hivyo mwenzangu aliamua kufanya maamuzi yake.”

KUTAKA KUJIUA

Anasema kitendo cha mkewe kudai talaka kilimfanya aingiwe na hofu kwamba pengine mkewe amepata mtu mwingine hivyo anataka kuwa huru, jambo ambalo lilimzidishia ‘stress’.

“Yaliponitokea hayo nilikuwa sioni sababu ya kuendelea kuishi kwa kweli sikufikiria mbali kabisa niliona ni bora nife tu, niliona kifo ndiyo suluhisho, sikujali familia yangu wala watoto, kiukweli nilichanganyikiwa sana sikuwa na mwanzo wowote wa maisha, maisha yangu yaliharibika ghafla, hadi nikitembea ama kukaa nilijikuta nazungumza peke yangu.

“Yeye alikuwa anataka nitoe talaka jambo ambalo sikuwa tayari kulifanya, mimi niliamua kumuoa, yeye anadai talaka, nikamwambia basi atoe yeye hiyo talaka kama inawezekana. Matokeo yake hivi sasa kila mtu anaishi kivyake, talaka haijatoka.”

TIPPO AOKOA MAISHA YAKE

Wakati amekata tamaa ya maisha na kujiona hafai kabisa kuendelea kuishi huku rafiki zake wakiwa bega kwa bega kumsaidia, mfanyabiasha maarufu nchini Tippo alichangia kumuweka sawa Masatu.

“Achana na rafiki zangu wengine walionibeba wakati nipo kwenye kipindi kigumu, lakini Athuman Tippo alinisaidia sana, kila muda alitaka niwe pamoja naye maana alijua naweza kufanya maamuzi gani. Mambo mengi Tippo aliyafanya kwa ajili yangu ili mradi tu nikae sawa, kiukweli namshukuru sana pamoja na rafiki zangu wote waliokuwa nami bega kwa bega wakati huo nimekata tamaa, sina hali yoyote.”

AZIM DEWJI AMPA DILI

“Kuna siku nilikuwa napitapita zangu Posta kule, niliingia kwenye mgahawa mmoja ndipo nilionana na mfadhili wangu wa zamani Azim Dewji, alistuka kuniona, aliniuliza nafanya shughuli gani nikamweleza sina kazi yoyote, akanihoji maswali mengi na kunitaka niende ofisini kwake akanipe kazi.

“Kweli siku niliyoambiwa niende nilienda na siku hiyo hiyo nilikabidhiwa gari ambapo aliniambia nichague gari lolote la kuendesha kama ni kwenda mikoani ama hapa hapa, nami nilichagua hapa, magari makubwa nilikataa.

“Hivyo kuanzia hapo maisha yangu sasa yalianza kubadilika kwani napata mshahara na ninaweza kuendesha maisha mwenyewe.

“Kupitia ajira hii nimeweza kununua viwanja huko Kigamboni (anatoa hati za viwanja hivyo) ambavyo ni kwa ajili ya wanangu maana mimi sina mpango wa kujenga kwasasa, nitaishi kwenye nyumba za kupanga maana sina familia, wanangu ndiyo wanapaswa kutengeneza familia zao,” anafafanua Masatu.

Dewji ambaye alikuwa mfadhili wa Simba miaka ya nyuma amekuwa bega kwa bega na mchezaji huyo kwani hata alipoumia mguu akiwa na timu ya taifa alichukua jukumu ya kumtibu kwa gharama kubwa.

Dewji aliamua kuchukua jukumu hilo baada ya Masatu kusikia maumivu makali huku ndugu zake wakitaka kumpeleka kwa mganga wa kienyeji visiwa vya Ukerewe, lakini haraka alitumiwa tiketi ya ndege ili aje kutibiwa Muhimbili na safari ya kwa mganga iliishia hapo.

“Unajua Azim Dewji amekuwa na msaada mkubwa katika maisha yangu, nakumbuka wakati huo nilipoumia mguu alitoa pesa yake kunitibu, niliumia nikiwa timu ya Taifa, majeraha ambayo yalinifanya nisuse kuitumikia timu hiyo kwani sikupata msaada, hata hivyo, baadaye Dewji aliniomba nirejee kikosini Stars.”

WATOTO SITA

Masatu ana watoto sita wa kike, kati ya hao mmoja alimzaa akiwa Indonesia hivyo anaishi huko ila kwa hapa Tanzania wapo watano.

Anasema akiwa katika kipindi cha ‘stress’ cha kuishi mbali na mkewe, alipata watoto wawili mwanamke mmoja, ambaye bahati mbaya akafariki na kisha akapata watoto wengine wawili na mwanamke wa pili ambaye naye akafariki pia.

“Wakati mwingine najiona mtu mwenye mkosi. wanawake wawili niliozaa nao wamefariki.

“Ila nashukuru wanangu ndiyo faraja yangu. Hawa wa hapa wote nimewanunulia viwanja huko Kigamboni na Mbagala Majimatitu ila huyo mmoja wa kwanza anayetarajia kuolewa niliyezaa na mke wangu, zawadi yake ya kiwanja nitampa siku ya ndoa yake, hivyo hata nikiondoka kesho kila mtoto atakuwa na sehemu yake, nimenunua viwanja vinne baada ya kupata kazi.

DEGREE YA MWANAYE

“Mtoto wangu wa kwanza bado anaishi na mke wangu ingawa alijitahidi sana kuniweka mbali naye ila namshukuru Mungu na ndugu zake waliingilia hilo, hata zile pesa ambazo nilikuwa nazituma hazikuniuma sana pamoja na mambo yaliyonipata kwani alijitahidi kumsomesha mwanangu ana degree moja, kwa kweli amemsomesha vizuri, anaitwa Sandrahope George Masatu.

“Huyo mwanangu anatarajiwa kuolewa mwezi Juni ingawa sitahudhuria ndoa yake bali nitatoa zawadi ya kiwanja ambacho kipo Kigamboni,” anafafanua Masatu.

MKEWE AMUUGUZA MKWE

Masatu anasema wakati baba yake anaumwa, mkewe alikuwa anatoa huduma kama kawaida japokuwa kwa usiri mkubwa.

“Wakati mzee wangu anaumwa kumbe mke wangu alikuwa akimuhudumia pasipo mimi kunishirikisha, nikaja kuambiwa hapo baadaye kuwa alihusika kuuguza na aliwaambia ndugu zangu wasiniambie, ingawa sasa hivi baba yangu ni marehemu.”

ANAISHI KISELA

Kutokana na mambo yaliyompata kwenye ndoa yake, Masatu ameweka wazi; “Siwezi tena kumwamini mwanamke kwa asilimia 100, hata hapa kwangu naishi pekee yangu, maisha yangu yatakuwa hivi hivi tu kikubwa wanangu nawasiliana nao na ninawapenda sana.

“Siwezi kumlaumu mtu bali ni familia yangu mwenyewe ambayo pia si ya kuilaumu sana.

“Sina mpango wa kuoa kabisa, nina mpenzi ila sina mpango wa kumuoa hata yeye nimemfahamisha kwamba akipata mtu wa kumuoa ni ruhusa wala simzuii.

“Mambo mengi yaliyonitokea kwenye mahusiano ndiyo yanayofanya nisitamani kuoa tena, unajua nilimwamini na kumpenda sana mke wangu, lakini ilifikia hatua nilikuwa najiwa na fikira mbaya.”

Usikose kusoma Mwanaspoti kesho Jumatano ambapoMasatu atafunguka kuhusu ushirikina ndani ya Simba.