Fury kustaafu ngumi

Muktasari:

Lakini wakati dunia ikisubiri pigano hilo la mabondia ambao hawajawahi kupoteza kabla ya pigano hilo, bondia mbishi Tyson Fury wiki hii amefichua kuhusu kuachana na ngumi kwa sababu ambazo hajaziweka wazi na tayari ameshatangaza kung’atuka!

JUMAMOSI hii hapa mwanangu! Ndani ya ukumbi wa MGM Grand uliopo Las Vegas nchini Marekani mabondia wawili wabishi Tyson Fury na Deontay Wilder watakunjana tena kwa mara ya pili baada ya awali kushindwana.

Vitasa baina yao hiyo Jumamosi vitakuwa ni kumaliza ubishi wa nani zaidi ya mwenzake ambapo tofauti na walivyotoka sare ya pointi 113-113 kwenye pigano la kwanza mwaka 2018, safari hii kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana mbabe.

Lakini wakati dunia ikisubiri pigano hilo la mabondia ambao hawajawahi kupoteza kabla ya pigano hilo, bondia mbishi Tyson Fury wiki hii amefichua kuhusu kuachana na ngumi kwa sababu ambazo hajaziweka wazi na tayari ameshatangaza kung’atuka!

Ndio, Fury ameweka wazi kuwa ataachana na masumbwi baada ya kupigana mapambano mawili baada ya hili la Jumamosi dhidi ya mpinzani wake mkubwa Deontay Wilder hii ikimaanisha kwamba ataachana na ndonga baada ya mapambano matatu tu yajayo.