Fully Maganga amenogewa kuiua Simba

Muktasari:

Magamba amekuwa na Ruvu Shooting tangu 2016 na kuwa na mafanikio katika mechi zinazoihusu timu yake na mabingwa hao wa soka nchini.

 

Dar es Salaam. Inaweza kuwa bahati, lakini kwa Fully Maganga ni zaidi ya neno hilo linapokuja suala la kuifunga Simba.

Maganga ndiye aliyepeleka ‘msiba’ mwingine kwa Simba katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuifanya Simba kuendelea kubaki nafasi ya nne ya msimamo ikiiacha Azam FC kuendelea kushikilia usukuani, huku mahasimu wao, Yanga wakiwa nafasi ya pili.

Matokeo ya jana yamemfanya Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck kuwa katika wakati mgumu klabuni hapo kwani ni kipigo cha pili mfululizo.

Lakini kwa Maganga ni kicheko, kwani ameendeleza ubabe wake kwa miamba hiyo ya soka nchini, akikumbuka baadhi ya mabao aliyoifunga Simba na kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliyowafunga mabingwa hao mara nyingi.

maganga aliifunga Simba mwaka huu katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi msimu uliopita, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, akiisawazishia timu yake.

Rekodi zinaonyesha Maganga amekuwa mwiba kwa makipa na mabeki wa Simba kwani hata wakati akiichezea Mgambo JKT (kabla haijashuka daraja) kuanzia 2012 hadi 2016, alikuwa na bahati ya kuifunga timu hiyo ya Kariakoo.

Aliiongoza Mgambo JKT kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Februari 9, 2014 pia alifunga bao moja kati ya mawili yaliyoipa Mgambo ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba kwenye mchezo uliochezwa Machi 18, 2015. Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Ally Nassor.

Pia, Maganga aliifungia Mgambo JKT bao la kufutia machozi katika mchezo uliofanyika Februari 3, 2016, ambao walipokea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Simba.

Nyota huyo alisema hakuna kingine kinachomfanya awe na uwezo wa kuifunga Simba zaidi ya kujiamini na kuongeza umakini awapo eneo la hatari.

“Nimekuwa najiamini kuwa naweza lakini pia nakuwa makini ninapokuwa eneo la hatari la timu pinzani, ndiyo maana nimekuwa nikifunga,” alisema Maganga.

Kipigo kimeacha maswali

Kocha Sven amebaki katika wakati mgumu baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo kwenye Ligi Kuu tanzania Bara, tukio ambalo halikuwa kutokea tangu msimu wa 2014/15.

Kukosekana kwa Meddie Kagere, Clatous Chama na Chris Mugalu kunaonekana kuwa tatizo katika kikosi cha Simba, ambacho hakijafunga bao lolote katika michezo miwili sasa na kuruhusu mawili.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji alionekana mwenye mawazo baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa juzi akimtumia Ibrahim Ajib kama mshambuliaji namba tisa, huku Charls Ilanfya akikosekana. Alimwanzisha pia Pascal Wawa na kumwacha nje, Benard Morrison alyeingia kipindi cha pili.

“Sikumbuki mara ya mwisho ni lini kwa Simba kufungwa mechi mbili mfululizo, lakini nawaomba radhi mashabiki kwa matokeo haya,” alisema Sven.

Mchambuzi wa soka nchini, mwalimu Alex Kashasha alisema kocha Sven anatakiwa kufanya mzunguko wa wachezaji ili kuwawekea mazingira ya kujiamini.

“Lazima awe na falsafa zaidi ya mbili.Simba ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini tatizo kubwa ni kucheza kwa staili moja kila wakati. Pasi fupi kila mara ili watu wapige makofi,” alisema.

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema mpango alioingia nao kocha wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa wa kujilinda ulikuwa sahihi kuliko ule wa Simba.

“Ruvu walijifunza Simba ilipocheza na Prisons, wakaingia kwa mipango ileile ya kujilinda, ndiyo maana unakuta kila Simba walipokuwa na mpira wao walikuwa wapo sita hadi saba eneo lao la 18 na kuwapa Simba wakati mgumu wa kufunga,” alisema Mayay, ambaye kwa sasa ni mchambuzi.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, mahasimu wao wanazidi kujiimarisha chinbi ya kocha mpya, Cedric Kaze, ambaye ameiimarisha katika nafasi ya pili.

Azam, ambayo ililala kwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar imeiacha Yanga kwa pointi mbili, yenye mchezo mchezo mkononi.