Fred,Fernandes wamsukumia nje ya kikosi Pogba

Muktasari:

Hafai kwa sababu haionekani kama Man United inashida tena ya huduma ya Pogba kwa hivi sasa. Mbrazili, Fred amekuwa si kichekesho tena na mashabiki wa Man United wanaamini atashindania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwenye klabu hiyo mwisho wa msimu.

MANCHESTER,ENGLAND. MINO Raiola, Ole Gunnar Solskjaer wapo kwenye vita ya maneno. Ugomvi wao mkubwa ni kuhusu hatma ya kiungo Paul Pogba.

Raiola anang’ang’ana kumwondoa Pogba kutoka Old Trafford. Solskjaer anamjibu kwamba hilo haliwezi kutokea hadi yeye apange.

Imekuwa vuta nikuvute kiasi cha kuwaingiza kwenye vita. Wakala anataka mteja wake aondoke, kocha anagoma na kuweka msimamo wa kumbakiza Manchester United.

Beki wa zamani huko Old Trafford, Gary Neville amemwambia Solskjaer ampige tu bei Pogba ili kuepukana na malumbano yasiyokuwa na maana dhidi ya Raiola.

Kitu cha aina hiyo kilisemwa pia na kiungo na nahodha wa zamani wa miamba hiyo, Roy Keane, aliyesema njia sahihi ya kumaliza malumbano ya kurushiana maneno baina ya Raiola na Solskjaer ni Man United kuchukua uamuzi wa kumuuza kiungo huyo.

Atauzwa, hauzwi? Lakini, je Man United wanashida na huduma ya Pogba kwa sasa? Maswali mengi yenye majibu tofauti. Pogba bado anafaa Man United, lakini pia hafai. Kila moja lina sababu zake.

Hafai kwa sababu haionekani kama Man United inashida tena ya huduma ya Pogba kwa hivi sasa. Mbrazili, Fred amekuwa si kichekesho tena na mashabiki wa Man United wanaamini atashindania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwenye klabu hiyo mwisho wa msimu.

Nemanja Matic amekuwa ukuta mgumu kwenye sehemu ya kiungo ya kukaba. Ingizo jipya la Solskjaer kwenye kiungo kwa kumleta Bruno Fernandes kumefanya timu hiyo kuwa na ufundi kuanzia kwenye sehemu ya katikati ya uwanja huko Scott McTominay akitarajia kurejea uwanjani hivi karibuni. Viungo hao wanne wote wanampa Solskjaer anachokitaka. Pogba wa kazi gani sasa jamani?

Kwenye mitandao ya kijamii huko, chaneli za Paul Pogba amekuwa bize wiki za karibuni akionyesha mazoezi anayofanya kwamba, kupona haraka kurudi uwanjani ndio kipaumbele chake.

Pogba amekuwa akionyesha kufanya mazoezi ya kila aina, mara kunyoosha miguu, kupiga pull-ups, kunyanyua vitu vizito na mambo mengine yanayohusu mazoezi ya kujiweka fiti.

Hii ni kama vile Pogback II baada ya ile ya mwanzo ya Pogback I, wakati aliporejea Old Trafford kutoka Juventus kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo ya Pauni 89 milioni mwaka 2016.

Pogba anahangaika kupona haraka majeruhi yake ya upasuaji wa enka ambayo yamemfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu msimu huu.

Hata kama hajacheza kwa muda mrefu, Pogba si kwamba hatakiwi kwenye kikosi hicho cha Man United na kocha wake, Solskjaer alisema: “Paul amekuwa na msimu mbaya wa kuandamwa na majeruhi na raha yake ni kucheza mpira.”

Hayo yalikuwa maneno ya Solskjaer mwezi uliopita kabla ya kutibuana na Raiola na kuongeza. “Kama kuna kitu kimoja ninachokifahamu kuhusu Paul basi ni kwamba, anapenda kucheza mpira na kufanya mazoezi. Namwona kabisa alivyochoshwa na kuwa majeruhi.”

Hilo ni jambo zuri, lakini unaambiwa hivi hata kama Pogba atapona kabla ya msimu huu kumalizika na kutaka kurudi kwenye timu, hatakuwa na uhakika wa kuanzishwa kwenye kikosi kutokana na viungo wa Man United wanavyopiga mzigo kwa sasa.

Pogba analazimisha kutaka kurudi akiamini kwamba atapata nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye kikosi, acheze apate nafasi ya kwenda Euro 2020 akiwa na Ufaransa.

Apate nafasi acheze kuzishawishi timu zinazohitaji huduma yake kuja kumsajili kwenye dirisha la majira ya kiangazi kama anavyohitaji wakala wake, Raiola.

Lakini, kwa bahati mbaya kwake, Man United na Solskjaer wanaonekana wameshasonga mbele wakati yeye alipokosekana kwenye kikosi. Wameshafidia kukosekana kwake na wanaonekana kutulia ndani ya uwanja bila hata huduma yake, wapo vizuri zaidi.

Kiwango cha soka walilocheza Jumatatu iliyopita waliposhinda 2-0 nyumbani kwa Chelsea, wakibeba pointi tatu zinazowafanya kuwa kwenye wakati mzuri wa kuifikia Top Four kwenye Ligi Kuu England, huo ulikuwa uthibitisho kwamba wanaweza kutimiza melango yao bila ya huduma ya Pogba waliyemsajili kwa Pauni 89 milioni.

Ubora wa Fred na Matic uwanjani Stamford Bridge wakati walipoikamatia sehemu ya kiungo na muda wote kuifanya Man United kuwa na mpira, ilionyesha dhamira ya dhati ya timu hiyo kwenye mpango wao wa kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Fred ameshabadili upepo na amekuwa si kichekesho tena kama ilivyokuwa awali wakati alipotua katika kikosi hicho kwa ada ya Pauni 52 milioni akitokea Shakhtar Donetsk.

Kucheza mfululizo kwenye Ligi Kuu England kumemrudisha Fred kwenye ubora wake na sasa Solskjaer hawezi kuthubutu kumweka nje ya uwanja. Solskjaer pia hatathubutu kumweka nje ya uwanja Matic. Ni hivyo pia kwa Fernandes na McTominay atakarudi uwanjani. Sasa Pogba atacheza wapi? Hakuna namna, itamlazimu kuanzia tu benchi.

Fred hana ule ufundi wa Pogba au nguvu nyingi za kupambana, lakini ukweli ndani ya miezi mitatu au minne iliyopita, amekuwa moto wa sehemu ya kiungo ya Man United.

Huko Stamford Bridge, Matic aliingizwa kikosini kuifanya Man United kucheza na viungo watatu na hakika ulikuwa mfumo ambao ulimpa faida kubwa Solskjaer. Matic na Fred wamekuwa na maelewano mazuri kwa siku za karibuni. Huko nyuma, Fred alikuwa akicheza na McTominay, ambaye pia walikuwa wakielewana vyema pia ndani ya uwanja. Bila shaka, McTominay akipona, atakuja kuendeleza kombinesheni yake na Fred, huku Matic akiwa mtu wa kuwasaidia kutokea kwenye benchi.

Kiungo mpya, Bruno Fernandes - amekuja kuonyesha kitu kimoja kwenye kikosi. Mechi mbili alizocheza, tayari zimeonyesha bayana kwamba humtarajii kuona Solskjaer akimweka benchi na ameshaanza kuwavutia mashabiki wa Man United.

Kutokana na hilo, Pogba sasa atacheza wapi? Bila ya shaka, benchi linamhusu atakaporudi kwenye kikosi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, ambapo mechi zake mbili za mwisho alicheza dhidi ya Watford na Newcastle United Krismasi huko.

Ni kitu cha wazi, kwanini Solskjaer aharibu safu yake ya kiungo ambayo imemfanyia kazi kwa karibu msimu wote kwa ajili ya kumpatia nafasi Pogba, mtu ambaye bila ya shaka mwisho wa msimu ataondoka?

Vita ya maneno baina ya Solskjaer na Raiola, inaonyesha wazi kinachosubiriwa ni msimu tu umalizike na dirisha la usajili wa majira ya kiangazi lifunguliwa ili mchezaji huyo aondoke. Hapo mkataba wake utakuwa umebaki mwaka mmoja na Juventus na Real Madrid zinaonekana kutaka saini yake. Man United sasa inafikiria kunasa viungo wengine kama Jack Grealish na James Maddison hiyo ilionyesha kwamba hawana tena mpango na Pogba, wanafikiria kitu kipya hasa ukizingatia kwamba maisha yanakwenda bila huduma yake.