Francis Kifukwe: kuweni watulivu tamko zito laja

Muktasari:

  • Kifukwe Yanga ndio mwenye uamuzi wa nani anatakiwa kuwaongoza hivyo wanachama ambao ndio wanapitisha nani anatakiwa kuwaongoza wanatakiwa kusikiliza viongozi wao wanasema nini na sio TFF.

MJUMBE wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Francis Kifukwe amewaomba wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu na kufuata katiba inayowaongoza, huku akiwataka kuachana na matamko yanayotolewa na Shirikiso la Soka Tanzania (TFF).

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na mchakato wa uchaguzi unaoendelea, Kifukwe alisema wanaotakiwa kusikilizwa zaidi na kufuatwa ni Wanayanga wenyewe kwani ndio waamuzi wa kila kitu katika klabu na sio TFF ambao wamekuwa wakiwayumbisha.

Alisema hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, George Mkuchika alithibitisha kuwa Yusuf Manji anaendelea kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo na TFF imesema haimtambui hivyo klabu ndio inatakiwa kusikilizwa kwa sababu ndiyo iliyompitisha na sio shirikisho.

“Sitaki kuzungumza mengi zaidi katika hilo kwa sababu mimi nipo katika Bodi ya Wadhamini na Mwenyekiti wangu ndiye aliyepitisha uwepo wa Manji hivyo naomba lijulikane hilo lakini hivi karibuni kutakuwa na tamko zito kutoka Yanga naomba ulisubiri hilo,”

“Nikikwambia ni tamko gani sasa nitakuwa nakiuka, tusubiri tutajua ni nini kitazungumzwa pia siwezi kukufahamisha kuwa ni tamko zuri au baya linaweza likawa zuri kwangu na kwako likawa baya hivyo kuwa na tusubiri,” alisema mjumbe huyo.