Fountain Gate yaipigisha kwata Transit Camp

Muktasari:

Ushindi walioupata timu hiyo ni wa tatu mfululizo wa ligi daraja la kwanza.

Morogoro. Mabao ya Salum Ngadu na Offen Chikola yamewapa ushindi wa mabao 2-0 timu ya Fountain Gate mbele ya maafande wa Transit Camp, mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Bao la kwanza la Salum Ngadu lilikuwa la mkwaju wa penati dakika ya 20, iliyotokana na beki mkongwe Damas Makwaya kuunawa mpira uliopigwa na Ngadu ambaye alifanikiwa kufunga penati hiyo.

Bao la pili lilitokana na kazi nzuri ya mshambuliaji Razack Omary aliyepiga shuti kali ambalo lilimbabatiza kipa Abdulrazack Ally kabla ya kugonga mwamba na kumaliziwa vema na Offen Chikola dakika ya 84.

Transit Camp walikuwa na nafasi nzuri ya kurudi mchezoni kufuatia penati waliyopata ambayo hata hivyo Ally Shomary alishindwa kufunga baada ya penati hiyo kupanguliwa na kipa Mussa Webilo.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Benedict Magali wa Mwanza, unaifanya Fountain Gate kuongoza kundi B kwa pointi tisa.

Kocha Mohammed Muya wa Fountain Gate, alisema ushindi huo umewaongezea kasi ya kufikia malengo yao ya kupanda ligi kuu.

"Nimefurahishwa na  ushindi huu kwa timu yangu ambao umetuongezea sababu za kufikia lengo la kucheza ligi kuu msimu ujao" alisema Muya.

Fountain Gate ambao wametumia Uwanja wa Jamhuri Morogoro baada ya ule wa Jamhuri Dodoma kuwa na matumizi mengine, mchezo ujao itawafuata vibonde Singida United.